2014-03-01 09:27:34

Uchunguzi unafanywa kuhusu uhakika wa miili ya Mapadre waliotekwa nyara DRC!


Hadi sasa hakuna habari za uhakika kuhusu mahali walipo Mapadre watatu wa Shirika la Assumption waliotekwa nyara kunako Mwezi Oktoba, 2012 nchini DRC. Habari zisizothibitishwa bado zinabainisha kwamba, kuna kaburi la pamoja ambalo limegunduliwa likiwa na masalia ya mwili wa Padre Jean Pierre Ndulani ambaye kwa miaka kadhaa alikuwa anatekeleza utume wake nchini Scotland na mwaka 2012 akarejea nchini kwao na hapo akakumbana na mkasa wa kutekwa nyara na watu wasiojulikana hadi leo hii.

Akizungumza na Shirika la Habari za Kimissionari, FIDES, Askofu Melchisedech Sikuli Paluku wa Jimbo Katoliki Butembo-Ben, mahali ambako Wamissionari watatu waliotekwa nyara walikuwa wanafanya shughuli zao za kichungaji anasema, kuna haja kwa watu kuvuta subira kwani kuna makuburi mawili yaliyopatikana yakiwa na miili kadhaa, lakini haijafahamika ikiwa kama kuna miili pia ya Mapadre waliotekwa nyara. Viongozi wa Kanisa wanaendelea kufanya uchunguzi wa kina ili kubainisha ukweli wa mambo.

Wamissionari waliotekwa nyara ni Padre Jean Pierre Ndulani, Padre Anselme Wasikundi pamoja na Padre Edmond Bamutute, walitekwa nyara hapo tarehe 21 Oktoba 2012 walipokuwa katika Parokia ya Notre Dame des Pauvres, Kilometa 70 kutoka Makao makuu ya Jimbo Katoliki la Butembo Beni, lililoko nchini DRC.







All the contents on this site are copyrighted ©.