Waraka wa Injili ya Furaha uwe ni mwongozo wa tafakari ya Kwaresima 2014
Kardinali Agostino Vallini, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma, anawaalika Maparoko wote
kufanya tafakari ya kina na hatimaye kuwashirikisha utajiri unaofumbatwa katika Waraka
wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko "Evangelii Gaudium", Injili ya Furaha katika
kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2014.
Kipindi hiki
kinaanza kwa kupakwa majivu, alama ya toba na wongofu wa ndani, hapo tarehe 5 Machi
2014. Hayo yamo kwenye barua ambayo Kardinali Vallini amewaandikia Maparoko wa Jimbo
kuu la Roma. Kwaresima kiwe ni kipindi cha kufanya tafakari ya kina kuhusu Waraka
wa Kitume ulioandikwa na Baba Mtakatifu Francisko katika kufunga Mwaka wa Imani sanjari
na kujikita katika Uinjilishaji Mpya.
Waraka huu una utajiri mkubwa wa kichungaji
unagusa kwa namna ya pekee tema muhimu zinazopaswa kufanyiwa kazi katika mchakato
wa Uinjilishaji Mpya. Waraka huu unaweza pia kuwa ni chimbuko la mipango na mikakati
ya shughuli za kichungaji kwa Parokia mbali mbali Jimbo kuu la Roma kwa kujikita katika
dhana ya Kanisa la Kimissionari, changamoto inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko
katika Mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo.