Dhamana na utume wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu, mwelekeo mpana wa utume
wa Baraza mintarafu mpango wa Mungu, Kanisa la Kitume ni chemchemi ya Sakramenti ya
daraja takatifu; Askofu anapaswa kuwa ni shahidi wa Kristo Mfufuka; Ukuu wa Mungu
katika uchaguzi wa Maaskofu wapya; Maaskofu wanapaswa kuwa ni wachamungu, watu wa
sala na wachungaji wema. Haya ni mambo makuu ambayo Baba Mtakatifu Francisko amekazia
kwa wajumbe wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu, wakati alipokutana nao, Alhamisi
tarehe 27 Februari 2014 mjini Vatican.
Baba Mtakatifu anasema, Kanisa linahitaji
viongozi wakweli na waadilifu; watu wanaoweza kujitosa kimasomaso kwa ajili ya watu
wa Mungu waliokabidhiwa kwao. Kanisa halihitaji mameneja, bali Askofu ambaye ni shahidi
wa ufufuko wa Kristo; mtu mnyenyekevu na jasiri; Kanisa halihitaji wapambanaji, bali
viongozi wanyenyekevu watakaopandikiza mbegu ya haki, ukweli na amani.
Baba
Mtakatifu amewakumbusha wajumbe wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu dhamana
na utume wao kwa ajili ya Makanisa mahalia kwa ajili ya kufanya uteuzi wa Maaskofu
wapya; wawe kweli ni watu walioteuliwa na Kristo kwa njia ya Roho Mtakatifu kwa ajili
ya Kanisa lake. Watu ambao watazingatia mahitaji ya Makanisa mahalia kwa kusoma alama
za nyakati. Askofu awe ni mtu mwenye uwezo wa kuunganisha nguvu na rasilimali iliyopo
kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Jimbo husika. Ustawi na maendeleo ya Kanisa yanategemea
kwa kiasi kikubwa uteuzi wa Maaskofu mahalia.
Baba Mtakatifu anasema hakuna
Askofu ambaye anaweza kukidhi viwango vinavyohitajika kwa kila Kanisa mahalia, kwani
kila Jimbo lina mazingira na changamoto zake zinazopaswa kufanyiwa kazi kwa ukamilifu.
Hapa kuna haja kwa Baraza la Kipapa lililopewa dhamana hiii kuvuka hali ya upendeleo,
mvuto na mguso wa mtu, mahali anapotoka mtu au mielekeo mbali mbali ya kijamii ili
kukidhi matakwa ya Mungu kwa ajili ya watu wake. Kanisa linahitaji Maaskofu wenye
mwono na mwelekeo mpana zaidi wa Mungu, na wala si watu wanaotishwa na malimwengu.
Baba
Mtakatifu anawataka wale wanaofanya kazi katika Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu
kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia: weledi, huduma na utakatifu wa maisha. Wanaweza
kupata dira na mwanga wa kufanya uchaguzi wa Maaskofu wapya kwa kufanya rejea kwenye
msingi wa Kanisa la Kitume, kwani ustawi na maendeleo ya Kanisa daima uko kwenye msingi
wake wa kitume kwa kujenga na kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwa Watu wa Mungu.
Huu ndio mwendelezo wa Mapokeo ya Kitume unaooneshwa miongoni mwa Maaskofu. Watu wamekwishaonja
katika hija ya maisha yao madhara ya utengano, sasa wanataka kuona Kanisa ambalo limeshikamana
katika umoja na udugu.
Baba Mtakatifu anasema, Askofu anapaswa kuwa ni shahidi
wa Kristo Mfufuka. Shahidi ambaye anashikamana na Kanisa na maisha yake ya kitume
na shughuli za kichungaji hayana budi kuwa ni kielelezo amini cha Kristo Mfufuka.
Awe na ujasiri wa kuyamimina maisha yake kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, kwani
hivi ni sehemu ya vinasaba vya Askofu wa Jimbo.
Askofu awe ni mtu mwenye uwezo
wa kuyasadaka maisha yake, kwani Uaskofu si mali yake binafsi bali ni kwa ajili ya
Kanisa na Kondoo aliokabidhiwa na Mama Kanisa; ni kwa ajili ya jirani zake na hasa
zaidi wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.
Baba Mtakatifu anasema, katika
mchakato wa kumtafuta Askofu haitoshi kuangalia sifa zake za kibinadamu: akili, uwezo
wake wa darasani au katika shughuli za kichungaji; haya ni mambo msingi lakini zaidi,
Askofu mtarajiwa hana budi kuwa ni mtu mkomavu wa kimaadili na utu wema; aliyefundwa
akafundika katika misingi ya maisha ya Kikristo; mwaminifu, mkweli, muwazi na mwenye
uwezo wa kuongoza kwa kuonesha dira na mwelekeo wa maisha kwa Familia ya Mungu atakayokabidhiwa.
Sifa hizi hazina budi kujionesha kwa namna ya pekee katika ushuhuda wa Kristo
Mfufuka, anayepaswa kupewa kipaumbele cha kwanza. Atambue wajibu na dhamana yake mbele
ya Mwenyezi Mungu na umuhimu wa kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwa Maaskofu
wengine. Mtu mwenye uwezo wa kufanya maamuzi na wengine na wala si kubaki peke peke
kama kisiwa! Baba Mtakatifu anakiri kwamba, si kila Askofu mtarajiwa anaweza kuwa
na sifa zote hizi kwa mkupuo! Jambo la msingi ni kuwa makini katika kufanya uteuzi
wa Maaskofu wapya.
Ukuu na utukufu wa Mungu unapaswa kupewa kipaumbele cha
kwanza na kwamba, uteuzi hauwezi kuchukuliwa kutokana na mtu kujisikia au uchunguzi
uliofanywa. Ili kuweza kuwa na uhakika wa maamuzi magumu yaliyopaswa kuchukuliwa,
anasema Baba Mtakatifu kuna haja ya mhusika kuweka wazi dhamiri yake mbele ya Mwenyezi
Mungu kwa kuzingatia umoja na mshikamano miongoni mwa Maaskofu.
Maaskofu hawana
budi kwanza kabisa kuwa ni watangazaji wa Habari Njema ya Wokovu kwani imani lazima
itangazwe. Kanisa linahitaji viongozi watakaolinda na kuendeleza Mafundisho tanzu
ya Kanisa yanayojikita katika upendo na uhuru kamili unaopata chimbuko lake kutoka
katika Injili. Kanisa haliwahitaji viongozi wanaojitafuta wenyewe au wanaopigana kulinda
masilahi yao binafsi; bali Kanisa linawataka watu wanyenyekevu na wasiopenda makuu;
watu wenye imani na wa kweli katika maisha yao, watu wanaotambua dhamana walioyokabidhiwa
na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya Kanisa.
Baba Mtakatifu anasema Askofu anapaswa
kuwa ni mtu mvumilivu anayetambua kwamba, kamwe magugu hayataweza kumea na kukua kiasi
hata cha kuharibu ngano bora iliyoko shambani. Askofu daima anapaswa kuwa ni mtu mwenye
imani na matumaini; mtu asiye ogopa kujisadaka kwani anatambua kwamba, hii ni kazi
ya Mungu ambayo imeanimishwa kwake. Kamwe Askofu hapaswi kujikatia tamaa, bali mtu
anayejiweka mbele ya Mungu daima kwa njia ya sala, kiasi hata za kujadiliana na Mungu
bila kuchoka, kwa hakika anasema Baba Mtakatifu Kristo atamwonesha dira na njia ya
kufuata.
Baba Mtakatifu akizungumza na wajumbe wa Baraza la Kipapa kwa ajili
ya Maaskofu anasema, Kanisa linahitaji Askofu mkweli na mwaminifu; mhudumu wa Neno
na kwamba urithi mkubwa anaoweza kuliachia Kanisa mahalia si: dhahabu wala almasi,
bali utakatifu wa maisha. Maaskofu katika maisha yao, waoneshe ushuhuda wa utakatifu
wa Mungu uliojificha ndani mwao. Daima wawe ni watu wanaojisadaka kwa ajili ya Familia
ya Mungu bila ya kujitumbukiza katika mazoea yanayoweza kuwaharibia kazi na kuwafanya
kukimbia majukumu yao ya kichungaji kwa kuelemewa na mazoea.
Baba Mtakatifu
anasema, utume na dhamana ya Askofu unahitaji udumifu unaojidhihirisha katika maisha
ya kila siku. Waamini wapate nafasi katika moyo na maisha ya Askofu wao, kielelezo
cha Kristo na Kanisa lake. Kwa njia hii, Askofu ataweza kuzima kiu ya maisha ya kiroho
kwa watu wake. Hivi ndivyo Baba Mtakatifu alivyofanya rejea kwenye Mtaguso mkuu wa
Trento, ambao amewataka wajumbe wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Maaskofu kuufanyia
kazi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo. Baba Mtakatifu anahitimisha
hotuba yake ambayo imetoa dira na mwongozo kwa ajili ya kufanya uteuzi wa Maaskofu
wapya kwa ajili ya Makanisa mahalia. Ana uhakika kwamba, Yesu Kristo ataendelea kufanya
hija na Kanisa lake!
Hotuba hii imehaririwa na Padre Richard A. Mjigwa,
C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.