2014-02-28 11:24:49

Ratiba elekezi ya Ibada za Kipapa kwa Mwezi Machi na Aprili 2014


Mshereheshaji mkuu wa Ibada za Kipapa Monsinyo Guido Marini ametoa ratiba elekezi ya Ibada mbali mbali zitakazoadhimishwa na Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi cha Mwezi Machi na Aprili 2014. Baba Mtakatifu hapo tarehe 5 Machi 2014, Jumatano ya Majivu, siku ya kufunga, kusali na kufanya toba kama kielelezo cha mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima,

Baba Mtakatifu atafanya maandamano kutoka katika Kanisa kuu la Mtakatifu Anselmi kama kielelezo cha toba kuelekea kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Sabina, huko ataadhimisha Ibada ya kupakwa majivu na Ibada ya Misa Takatifu. Ibada hii itafanyika majira ya jioni, yaani Saa 10: 30.

Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Kwaresima hapo tarehe 9 Machi 2014, Baba Mtakatifu pamoja na wasaidizi wake wa karibu watafanya Mafungo ya kiroho mjini Ariccia na kuhitimishwa hapo tarehe 14 Machi 2014.

Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 16 Machi 2014 majira ya Saa 10: 00 jioni atafanya hija ya kichungaji Parokiani "Santa Maria dell' Orazione". Tarehe 28 Machi, Ijumaa, majira ya saa 11:00 jioni kwa saa za Ulaya, Baba Mtakatifu Francisko ataongoza Ibada ya Kitubio, kama sehemu ya hija ya Kipindi cha Kwaresima.

Jumapili tarehe 6 Aprili 2014, Baba Mtakatifu amepanga kutembelea Parokia moja ya Jimbo kuu la Roma kuanzia saa 10:00 jioni kwa saa za Ulaya.

Baba Mtakatifu Francisko, hapo tarehe 13 Aprili 2014, Jumapili ya Matawi na Siku ya Vijana Kijimbo, kuanzia saa 3:30 asubuhi atabariki matawi pamoja na kufanya maandamano kabla ya kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Tarehe 17 Aprili, Alhamis Kuu, Baba Mtakatifu Francisko kuanzia saa 3:30 asubuhi ataadhimisha Ibada ya Misa ya Krisma ya Wokovu, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Tarehe 18 Aprili, Ijumaa Kuu, Siku ya mateso na kifo cha Kristo, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Mateso ya Kristo kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Majira ya saa 3:15 Usiku atashiriki kwenye Njia ya Msalaba itakayofanyika kwenye Magofu ya Colosseo.

Tarehe 19 Aprili, Jumamosi kuu, katika Kesha la Pasaka, kuanzia saa 2: 30 Usiku, Baba Mtakatifu ataongoza Ibada ya Misa Takatifu. Jumapili tarehe 20 Aprili, Papa anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu na baadaye kutoa ujumbe wake kwa ajili ya Mji wa Roma na Dunia kwa ujumla, majira ya saa 6:00 Mchana.

Tarehe 27 Aprili, Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Pasaka, Maarufu kama Jumapili ya Msamaria mwema, Baba Mtakatifu anatarajiwa kuwatangaza Wenyeheri Yohane wa XXIII na Yohane Paulo II kuwa Watakatifu. Hili litakuwa ni tukio la kihistoria kuweza kufunga Mwezi Aprili, 2014 anasema, Monsinyo Guido Marini, Mshereheshaji mkuu wa Ibada za Kipapa mjini Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.