Ujenzi wa tasaufi ya umoja isaidie mchakato wa hija ya majadiliano ya kidini na kiekumene
Mshikamano wa upendo miongoni mwa wafuasi wa Kristo ndiyo kauli mbiu iliyoongoza mkutano
wa Maaskofu rafiki wa Chama cha Kitume cha Wafokolari kutoka sehemu mbali mbali za
dunia waliokuwa wamekutanika mjini Gastel Gandolfo. Ni tukio ambalo pamoja na mambo
mengine linalenga kujenga na kuimarisha umoja na udugu, kwa kushirikishana tunu msingi
za maisha ya kiroho na kichungaji mintarafu karama ya umoja wa Kanisa. Maaskofu wanapaswa
kutekeleza dhamana hii kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa zima.
Watu
wana kiu na hamu ya kutaka kuona na kusikia ushuhuda wa maisha ya watu ambao wamejitoa
bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake; ndugu wanaopendana na kuheshimiana
licha ya tofauti zao za tabia, mahali wanapotoka na umri wao. Mwelekeo huu unaibua
changamoto ya umoja na mshikamano wa Kanisa zima, kwani upendo wa Kristo una nguvu
ya kuweza kuleta maboresho ya nguvu katika mahusiano ya watu; watu wanasikia mwaliko
wa kumtambua Kristo kati yao, tayari kujiondoa kutoka katika ubinafsi wao, ili kukutana
na wengine, tayari kuwashirikisha matumaini waliyopokea kutoka kwa Kristo kama zawadi
kubwa!
Ni maneno ya Baba Mtakatifu Francisko wakati alipokutana na Kundi la
Maaskofu rafiki wa Chama cha Kitume cha Wafokolari, siku ya Alhamisi, tarehe 27 Februari
2014. Kanisa linapaswa kuwa ni nyumba na shule ya umoja, changamoto kubwa katika mapambazuko
ya Millenia ya tatu ya Ukristo, kwa kuendelea kuwa waaminifu kwa Kristo na kujibu
kwa umakini mkubwa kilio cha watu na mategemeo yao; jambo la msingi ni kujenga na
kudumisha kwanza tasaufi ya umoja na mshikamano.
Hiki kiwe ni kikolezo makini
cha elimu na majiundo ya maisha ya Kikristo; mahali ambapo wahudumu wa Mafumbo ya
Mungu, watawa na watekelezaji wa mikakati ya shughuli za kichungaji wanafundwa bila
kusahau sehemu zote zinazojikita katika majiundo makini ya maisha ya kifamilia na
Jumuiya ya Kikristo.
Baba Mtakatifu Francisko anabainisha kwamba, ujenzi wa
Kanisa kama nyumba na shule ya umoja ni kielelezo makini cha mikakati ya Uinjilishaji
Mpya, ili wote waweze kuwa wamoja chini ya Kristo. Hii ndiyo nguvu ya Roho Mtakatifu
inayookoa na kuleta mvuto. Ujenzi wa tasaufi ya umoja inasaidia katika mchakato wa
uimarishaji wa hija ya majadiliano ya kidini na kiekumene.
Baba Mtakatifu
amewashukuru Maaskofu rafiki wa Chama cha Kitume cha Wafokolari kwa kumtembelea mjini
Vatican, kama sehemu ya mchakato wa kujenga na kuimarisha mshikamano na umoja miongoni
mwa Maaskofu pamoja kukuza upendo na ujasiri wa matumaini mapya. Baba Mtakatifu Francisko
amewaambia Maaskofu hao kwamba, anatumainia sala zao katika maisha na utume wake kama
Khalifa wa Mtakatifu Petro.