2014-02-27 11:16:51

Sinodi za Maaskofu ni jukwaa makini la kukutana ili kusikiliza kilio cha waamini katika maisha na utume wao!


Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu anasema, Sekretarieti ya Sinodi ya Maaskofu imekwishapokea sehemu kubwa ya majibu ya maswali dodoso yaliyotumwa kwenye Mabaraza ya Maaskofu Katoliki, sehemu mbali mbali za dunia. Majibu haya yanaonesha kilio kikuu cha baadhi ya waamini wanaojisikia kwamba, wametengwa na Mama Kanisa kutokana na kujikuta wanaishi maisha ambayo ni kinyume cha Mafundisho, Sheria, Kanuni na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa.

Maadhimisho ya Sinodi Maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia iliyoitishwa na Baba Mtakatifu Francisko ni cheche za mwelekeo mpya wa Maadhimisho ya Sinodi unaoonesha mshikamano na umoja miongoni mwa Maaskofu katika kukabiliana na changamoto za kichungaji zinazoendelea kuibuliwa katika maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Majibu yaliyotolewa na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki, Vikundi na watu binafsi ni changamoto kubwa kwa Mama Kanisa kuwaendelea watu mahali waliko ili kuwasikiliza na kuwatekelezea yale yanayokera katika hija ya maisha yao ya kiroho na kiutu. Umefika wakati kwa viongozi wa Kanisa kuwaendelea watu wao huko waliko badala ya kutunga sera na mikakati ya kichungaji wakiwa wamejifungia ofisini kwao. Waguswe na kuonja hali halisi ya maisha na changamoto za watu mitaani, vigangoni, parokiani na majimboni.

Kardinali Lorenzo Baldisseri anasema kwamba, sehemu kubwa ya majibu ya maswali dodoso yaliyotumwa kutoka kwenye Mabaraza ya Maaskofu Katoliki yametolewa muhtasari, lakini bado Maaskofu wameonesha utajiri mkubwa wa majibu na mchango wa waamini na wote walioguswa na maisha na utume wa Kanisa katika masuala ya ndoa na familia kwenye tovuti za Mabaraza ya Maaskofu Katoliki. Hii inaonesha kwamba, watu wengi wameguswa na changamoto za maisha na utume wa Kanisa kwa ajili ya familia, kiasi cha kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kujibu maswali dodoso yaliyotumwa na Sekretarieti ya Sinodi ya Maaskofu.

Mchakato wa hija ya Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu umefungua ukurasa mpya wa majadiliano ya kina kati ya Kanisa na Waamini, kiasi cha kuanza kuona imani na matumaini kwa wale waliokuwa wameanza kuchoka na kujikatia tamaa ya maisha ya kiroho. Wengi wanasema wanaendelea kuchangamotishwa na Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ni kiongozi anayeguswa na mahangaiko ya watu sehemu mbali mbali za dunia.

Kardinali Lorenzo Baldisseri anasema, kwa sasa Sekretarieti imeanza kuandaa Hati ya Kufanyia Kazi, Instrumentum Laboris itakayotumiwa na Mababa wa Sinodi wakati wa Maadhimisho ya Sinodi Maalum ya Maaskofu.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuhimiza umuhimu wa Sinodi za Maaskofu katika maisha na utume wa Kanisa, kama kielelezo makini cha umoja na mshikamano miongoni mwa Maaskofu katika utekelezaji wa mikakati ya kichungaji ndani ya Kanisa. Ikumbukwe kwamba, Sinodi ya Maaskofu kuhusu Familia itaadhimishwa katika awamu mbili: Awamu ya kwanza inajadili matatizo na changamoto zinazojitokeza katika maisha na utume wa Kanisa kuhusiana na familia.

Awamu ya Pili itakayoadhimishwa mwaka 2015 itakuwa na dhamana ya kutoa mapendekezo kwa Khalifa wa Mtakatifu, ili aweze kutoa mwelekeo wa jumla kwa ajli ya maisha na utume wa Kanisa katika utume wa Ndoa na Familia. Makardinali wamejadili kwa kina na mapana kuhusu changamoto za maisha na utume wa Familia katika mwanga wa Uinjilishaji Mpya. Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia wanandoa na familia barua ya wazi, akiwataka kusali kwa ajili ya mchakato mzima wa Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu Familia wakitambua kwamba, wao ndio wahusika wakuu.

Hii ni changamoto kwa Maaskofu kujenga na kuimarisha mshikamano miongoni mwao na Mapadre ambao ni wasaidizi wao wa karibu katika kufundisha, kutakatifuza na kuwaongoza watu wa Mungu bila kuwasahau watawa na waamini walei. Changamoto za kichungaji zinazolikabili Kanisa katika ujumla wake zinapaswa kushughulikiwa katika mtazamo wa utume na dhamana ya Kanisa katika Uinjilishaji Mpya.







All the contents on this site are copyrighted ©.