Maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu Familia yapamba moto!
Sekretarieti ya Sinodi ya Maaskofu, hivi karibuni, imehitimisha mkutano wake wa kumi
na tatu, uliofanyika katika kipindi cha siku mbili. Mkutano huu umejadili pamoja na
mambo mengine, majibu ya maswali dodoso yaliyotumwa kwenye Mabaraza ya Maaskofu Katoliki
duniani kote kama sehemu ya Maandalizi ya Maadhimisho ya Sinodi Maalum ya Maaskofu
kwa ajili ya Familia itakayoadhimishwa mjini Vatican mwezi Oktoba, 2014.
Takwimu
zinaonesha kwamba, asilimia ya majibu yaliyotolewa ni kubwa na kwamba, kumekuwepo
pia na majibu yaliyotolewa na makundi pamoja na watu binafsi kutoka sehemu mbali mbali
za dunia. Kikao cha Sekretarieti, kilihudhuriwa pia na Baba Mtakatifu Francisko aliyekazia
kwa mara nyingine tena umuhimu wa Sinodi kama kielelezo makini cha umoja na mshikamano
wa Maaskofu kutoka sehemu mbali mbali za dunia sanjari na mada itakayojadiliwa kwenye
Sinodi ya Mwaka 2014 na ile ya Mwaka 2015.
Wajumbe wamefurahia majibu ya dodoso
ya maswali yaliyoulizwa na kwamba, hapa patakuwa ni mahali ambapo sauti ya Makanisa
mahalia itaweza kusikika mintarafu: maisha, utume, matatizo na changamoto za maisha
ya ndoa na familia; tayari kutweka hadi kilindini ili kutangaza Injili ya Familia,
licha ya changamoto na kinzani zinazojitokeza katika tunu msingi za maisha ya ndoa
na familia.
Majadiliano haya yatasaidia katika utengenezaji wa Hati ya Kufanyia
Kazi inayojulikana kwa lugha ya Kilatini kama "Instrumentum Laboris". Kuna uhusiano
wa dhati kati ya Maadhimisho ya Sinodi Maalum ya Maaskofu kuhusu Familia na Sinodi
ya Kawaida ya Maaskofu kuhusu Familia, Sinodi ambayo itatoa mapendekezo yatakayotumiwa
na Baba Mtakatifu katika kuandaa Waraka wake wa Kitume kwa ajili ya Kanisa la Kiulimwengu.
Mkutano
huu umehudhuriwa pia na Wawezeshaji wakuu wa Sinodi: Kardinali Peter Erdo pamoja na
Askofu mkuu Bruno Forte, Katibu maalum wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Familia.
Baba Mtakatifu Francisko alitumia fursa hii kubariki eneo jipya la Sekretarieti ya
Sinodi ya Maaskofu ambayo kwa sasa ina Kikanisa na Ofisi mpya ili kurahisisha utekelezaji
wa shughuli za Sinodi za Maaskofu.