Mwamini anayeimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara anapaswa kutolea ushuhuda wa imani
yake kwa Kristo na Kanisa lake pasi na woga wala makunyanzi. Mwamini ambaye kweli
ni mfuasi wa Kristo anafikiri na kutenda kadiri ya Kristo mwenyewe, hali inayoshuhudiwa
katika uhalisia wa maisha. Kama hakuna ushuhuda wa maisha ya Kikristo hapo kuna jambo
ambalo haliendi sawa sawa na linapaswa kushughulikiwa kikamilifu.
Ni sehemu
ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Maadhimisho ya Fumbo
la Ekaristi Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican
siku ya Alhamisi. Anasema, wakristo wanaoshindwa kushuhudia imani yao kwa Kristo na
Kanisa lake, hawalitendei vyema Kanisa. Watu wanaotumia mali na utajiri wao vibaya
kwa ajili ya kuwadhulumu na kuwanyanyasa maskini na wanyonge wanakwenda kinyume cha
Mafundisho ya Kristo na kwamba, kilio na mahangaiko ya watu hawa iko siku yatasikika
mbele ya Mwenyezi Mungu na wahusika watakiona cha mtema kuni! Anasa na tamaa za mwili
yamekuwa ni mambo yanayowafurahisha wengi lakini yanakwenda kinyume kabisa na njia
za Bwana. Hii ni kashfa.
Yesu katika Mafundisho yake anakemea kwa ukali kashfa
dhidi ya wadogo wanaomwamini na kwamba, kashfa zinamwelekeo wa kuua maisha ya watu
kiroho. Kuna haja anasema Baba Mtakatifu Francisko kuhakikisha kwamba, maneno na matendo
ya Wakristo yanashuhudiwa katika uhalisia wa maisha na wala si kinyume chake. Imani
ijioneshe katika matendo. Ushuhuda wa imani tendaji ni kikolezo hata kwa wale wasioamini.
Baba Mtakatifu anasema, kwa mtu asiye amini anavutwa zaidi na ushuhuda wa
matendo yanayoonesha mambo makuu yanayofumbatwa katika moyo wa mwanadamu. Imani bila
matendo, hiyo imekufa ndani mwake, hata kama mwamini atadiriki kusimulia Biblia nzima
kwa mtu asiye amini, bila matendo ni sawa na kumpigia mbuzi gitaa! Wakristo waoneshe
ushuhuda wa imani tendaji, hapo mambo yataweza kubadilika.
Baba Mtakatifu
anawaalika waamini kusali ili kuwaombea waamini waweze kutolea ushuhuda wa imani yao
katika uhalisia wa maisha ya kila siku. Pale waamini wanapojikuta wanaogelea katika
dimbwi la dhambi na mauti, wasisite kukimbilia upendo na huruma ya Mungu. Wakristo
waoneshe ujasiri wa kutubu na kumwongokea Mungu!