2014-02-27 09:30:51

Kanisa litaendelea kushikamana na maskini pamoja na kusimama kidete kwa ajili ya mafao ya wengi!


Kanisa linahamasishwa kuwa kweli ni mfano wa: unyofu, ukweli na uwazi; haki na amani; huruma na mapendo katika ulimwengu ambamo watu wanaendelea kukengeuka na kupotoka katika ukweli, maadili, utu wema, rushwa na ufisadi wa mali ya umma. Hii ni sehemu ya ujumbe kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki India baada ya kuhitimisha mkutano wake wa thelathini na moja, uliowashirikisha Maaskofu 187 kutoka katika Kanisa Katoliki nchini India. RealAudioMP3

Maaskofu wamejikita katika changamoto ya kufanya mageuzi makubwa katika maisha na utume wa Kanisa kama ambavyo anaendelea kuhimiza Baba Mtakatifu Francisko pamoja na kuhakikisha kwamba, Kanisa kweli linafungamana na maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Umefika wakati wa kumwilisha mafundisho makuu yaliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, miaka hamsini iliyopita, kwa kutambua kwamba, Kanisa ni Familia ya watu wa Mungu inayofanya hija ya kumwendea Yesu Kristo kama Jumuiya zinazoinjilisha. Kanisa halina budi kuendelea kusimama kidete na wote wanaoteseka na kusumbuka kutokana na mahangaiko mbali mbali ya mwanadamu kwa kuongozwa na kanuni msingi tatu: utu na heshima ya binadamu; mshikamano na majadiliano katika ukweli na uwazi kwa ajili ya mafao ya wengi.

Baraza la Maaskofu Katoliki India linapenda kuendeleza mbele juhudi za kuimarisha Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo kama shule ya Neno la Mungu, maisha ya Kisakramenti na Imani inayomwilishwa kwa njia ya matendo ya huruma kwa jirani na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo hazina budi kupata chimbuko na uhalali wake katika Tafakari ya Neno la Mungu na Adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu, ili kweli ziweze kuwa ni vyombo vya Uinjilishaji Mpya katika ulimwengu wa utandawazi!

Maaskofu Katoliki India wanasema, kuna haja kwa Kanisa kuhimiza umuhimu wa waamini kutafakari kwa kina na mapana, Neno la Mungu pamoja na kuchuchumilia maisha ya Kisakramenti kama njia muafaka za kukutana na kuzungumza na Mwenyezi Mungu. Mwaliko huu unahitaji kwa nmna ya pekee, toba na wongofu wa ndani, ili waamini waweze kuonja tena na tena huruma na upendo wa Mungu. Hata maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii wanapaswa kushirikishwa katika maisha na utume wa Kanisa.

Maaskofu wanasema, wataendelea kuwa ni sauti ya kinabii kwa wanyonge na watu wasiokuwa na sauti kwa kukemea na kulaani ukosefu wa misingi ya haki, amani na utulivu ndani ya Jamii sanjari na kuhimiza utekelezaji wa utawala wa sheria. Kanisa linapenda kujielekeza zaidi kwa kuwa sehemu ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Kanisa litaendelea kushikamana na wananchi wote wa India wanaonyanyasika kutoka na hali yao ndani ya Jamii na kwamba, litaendelea kupigania haki sawa kwa wananchi wote wa India. Kanisa katoliki nchini India linapinga sheria ya rais ya Mwaka 1950 inaonesha ubaguzi katika Jamii.

Baraza la Maaskofu Katoliki India katika mkutano wake, limekazia dhamana na nafasi ya waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa. Wanawake wanapaswa kuwezeshwa ili waweze kushiriki kikamilifu katika ustawi na maendeleo ya Kanisa nchini India. Maaskofu wanalaani vitendo vya nyanyaso za kijinsia vinavyofanywa dhidi ya wanawake na wasichana nchini India.

Maaskofu wanawaalika waamini walei kushiriki kikamilifu katika medani mbali mbali za maisha nchini India kama njia ya uwepo na ushuhuda wao makini unaopania kuyatakatifuza malimwengu kwa kukuza na kuendeleza pia majadiliano ya kidini na kiekumene kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi waƬote wa India. Majadiliano hayana budi kusimikwa katika uhalisia wa maisha.

Maaskofu Katoliki India katika ujumbe wao kwa watu wa Mungu wanawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa mstari wa mbele kulinda na kutunza mazingira pamoja na kushiriki katika mchakato wa sera na mikakati ya maendeleo endelevu kwa ajili ya mtu mzima: kiroho na kimwili.








All the contents on this site are copyrighted ©.