Jitokezeni kushiriki katika mchakato wa uchaguzi mkuu nchini Namibia
Baraza la Maaskofu Katoliki Namibia linawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi
mema nchini humo kujitokeza kwa wingi ili kushiriki kwenye mchakato wa uchaguzi mkuu
unaotarajiwa kufanyika nchini humo mwaka 2014. Wananchi wengi wamekwishaanza kujiandikisha
kama sehemu ya mchakato wa maandalizi ya zoezi zima la kupiga kura mwezi Novemba.
Maaskofu wanasema,
ushiriki wa wananchi katika mchakato wa upigaji kura ni muhimu katika kuimarisha zoezi
zima la demokrasia pamoja na utekelezaji wa haki na demokrasia shirikishi, ili hata
sauti ya wananchi iweze kusikika kwa njia ya kupiga kura. Hii ni haki ambayo wananchi
wa Namibia hawana sababu yoyote ya kuipuuzia. Waamini na wananchi katika ujumla wao
wanahimizwa kupiga kura kwa kuongozwa na dhamiri nyofu.
Baraza la Maaskofu
Katoliki Namibia linaitaka Serikali na Tume ya uchaguzi nchini Namibia kuhakikisha
kwamba, wanazingatia: ukweli na uwazi, kanuni na maadili ya uchaguzi mkuu. Tume iendelee
kuwahamasisha wananchi kushiriki katika zoezi zima la uchaguzi nchini Namibia pamoja
na kutoa elimu ya uraia. Kuna haja ya kuboresha pia daftari la wapiga kura na kwamba,
siku ya uchaguzi watu washiriki kikamilifu katika zoezi hili kwa uhuru, amani na utulivu.
Vyama na wagombea wote wahakikishe kwamba, wanazingatia sheria, kanuni na
maadili ya uchaguzi mkuu, ili uchaguzi uweze kuwa huru na wa haki. Wagombea wapewe
nafasi sawa katika vyombo vya habari ili waweze kufafanua sera na malengo ya vyama
vyao ikiwa kama wananchi watawapatia ridhaa ya kuongoza nchi ya Namibia.
Kwa
wale watakaoshindwa kwa uhalali wakubali matokeo. Baada ya uchaguzi vyama vya siasa
vihakikishe kwamba, amani, umoja na mshikamano wa kitaifa vinaendelezwa na kamwe wananchi
wasigawanywe kwa misingi ya kisiasa, kikabila wala udini. Ujumbe wa Baraza la Maaskofu
Katoliki Namibia umetiwa sahihi na Askofu mkuu Liborius Ndumbukuti Nashemba, Rais
wa Baraza la Maaskofu Katoliki Namibia.