Jengeni utamaduni wa kuheshimiana, kuthaminiana na kupendana, ili haki, amani na utulivu
viweze kushamiri!
Mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu, changamoto kubwa inayomkabilia
binadamu ni kupendana, kuheshimiana na kusaidiana kwa hali na mali. Kukosa na kukoseana
ni jambo la kawaida katika hija ya maisha ya binadamu, lakini kuanza kulipiza kisasi
ni kwenda kinyume kabisa cha mpango wa Mungu kwani kimsingi mwanadamu anakosa vigezo
vya kutekeleza haki kadiri ya mpango wa Mungu.
Kutokana na ukweli huu, mwanadamu
hana budi kuhakikisha kwamba, anaachana na tabia ya kulipiza kisasi. Mwenyezi Mungu
amewaumba binadamu katika tofauti kubwa, lakini wote wanapaswa kuishi kama Jumuiya
kwa kusaidiana, kwani hakuna mtu anayeweza kuishi kama kisiwa. Wakristo kwa namna
ya pekee wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha
mshikamano wa upendo kati yao na wale wote wanaowazunguka, ili kupandikiza mbegu ya
haki, amani na upatanisho wa kweli unaobubujika kutoka katika undani wa mtu!
Hii
ni changamoto iliyotolewa hivi karibuni na Askofu msaidizi Titus Mdoe wa jimbo kuu
la Dar es Salaam katika Ibada ya Misa Takatifu kwenye Parokia ya Bikira Maria wa Consolata,
Kigamboni. Askofu msaidizi Mdoe alikuwa Parokiani hapo ili kutembelea na kuzungumza
na Familia ya Mungu, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Ushuhuda wa maisha adili na amini
uwe ni mfano wa kuigwa na jirani wengine. Upendo kwa Mungu na jirani ni silaha madhubuti
dhidi ya vita, kinzani na migogoro ya kijamii inayoendelea kufuka moshi sehemu mbali
mbali za dunia na kama inavyojionesha pia nchini Tanzania.
Askofu msaidizi
Titus Mdoe anasema kamwe watu hawawezi kulingana, watatofautiana, lakini hawana budi
kujenga na kuimarisha utamaduni wa kupendana na kusaidiana kwa hali na mali kama ndugu
wamoja. Kuna watu wanaokabiliana na hali ngumu ya maisha ndani ya Jamii wakati huo
huo kuna kundi la watu wachache wanaoendelea kuvinjari na kuponda maisha.
Waamini
wanahamasishwa kujenga moyo wa kusamehe na kusahau, ili kuanza mchakato wa kujipatanisha
na Mungu pamoja na jirani zao, ili kujenga mazingira yatakayoiwezesha dunia kuwa ni
mahali pazuri zaidi pa kuishi. Watu wajitaabishe kufanya kazi halali ili kujipatia
mahitaji yao msingi na kwamba, hakuna njia ya mkato katika maisha kwa kujikita katika
imani za kishirikina zinazoendelea kusababisha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.
Utajiri unapatikana kwa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa.
Chuki na uhasama
wa kisiasa ni sumu inayoweza kukwamisha maendeleo ya watanzania wengi. Kumbe, watanzania
hawana budi kuhakikisha kwamba, wanaondokana na siasa zinazojenga chuki na uhasama
kati yao. Waongozwe na hoja ya nguvu na wala si nguvu ya hoja kama inavyojionesha
katika mikutano mingi ya kisiasa.
Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba linaloendelea
mjini Dodoma watambue dhamana kubwa waliyopewa na watanzania wenzao katika mchakato
wa kutafuta Katiba itakayokuwa ni Sheria Mama katika utekelezaji wa haki msingi za
binadamu, demokrasia na uhuru wa kweli; utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa
sura na mfano wa Mungu. Ustawi na maendeleo ya watanzania wote yapewe kipaumbele cha
kwanza badala ya kuangalia makundi ya watu wanayoyawakilisha kwenye Bunge hili maalum.