Wanandoa tokeni kifua mbele kuinjilisha na kuyatakatifuza malimwengu!
Huduma kubwa inayotekelezwa na Mama Kanisa kwa wanandoa wakristo ni kuwaita na kuwasindikiza
katika hija ya maisha na utume wao wa ndoa na familia, ili kutambua na hatimaye kushirikishana
ile furaha inayobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ndoa. Hii ni zawadi kubwa kwa
wanandoa Wakristo kutoka kwa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka katika wafu.
Katika ulimwengu
wa utandawazi, maendeleo ya sayansi na teknolojia, ni jukumu la wanandoa wenyewe kusimama
kidete na kutoka kifua mbele kwa ajili ya kuinjilisha na kuyatakatifuza malimwengu
kwa njia ya ushuhuda wa maisha adili yanayosimikwa katika imani, matumaini na mapendo
kwa Kristo na Kanisa lake. Ni wajibu wa Familia za Kikristo kuwa ni sehemu ya
Habari Njema kwa watu wa mataifa waliokata tamaa na kutopea katika ukanimungu, ili
watu wengine waweze kuonja ile furaha ya kufunga ndoa ya Kikristo, kama zawadi kubwa
katika maisha ya mwamini, tayari kushiriki katika kazi ya uumbaji ambayo Mwenyezi
Mungu amemkabidhi mwanadamu! Hivi ndivyo anavyoandika Askofu mkuu Francesco Pio
Tamburrino wa Jimbo kuu la Foggia-Bovino, Italia katika barua yake ya kichungaji,
kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilee ya miaka mia mbili tangu Jimbo hili lilipowekwa
chini ya ulinzi na usimamizi Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Familia ni
mada ambayo kwa sasa ni kati ya changamoto za kichungaji kwa Mama Kanisa wakati huu
wa Mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Wanandoa wanakumbushwa ile siku
ya furaha na vigelegele walipokuwa wamevalia mavazi meupe, wakimeta meta mbele ya
waamini na kupeana ahadi ya uaminifu na udumifu katika Sakramenti ya Ndoa, hadi pale
kifo kitakapowatengenisha. Lakini, jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, familia nyingi
za Kikristo kwa sasa zinakabiliana na majanga ya utengnano. Nchini Italia anasema
Askofu mkuu Francesco Pio Tamburrino, ndoa nyingi zinaweza kudumu kwa takribani miaka
kumi na tano, baada ya hapo, wanandoa wanachokana na kuanza kusakamana kwa vitimbwi
na hatimaye, ndoa yenyewe kuvunjika. Licha ya majanga yote haya familia bado ni nguzo
msingi ya maisha ya kijamii, ingawa kwa sasa kuna mitazamo hasi hata kuhusiana na
ndoa na familia. Hizi ni changamoto za kichungaji zinazofanyiwa kazi sasa na Mama
Kanisa, kwani kuna uhusiano mkubwa kati ya dhamana ya Uinjilishaji Mpya na Familia,
ndiyo maana, Baba Mtakatifu Francisko ameitisha Sinodi Maalum ya Maaskofu kwa ajili
ya Familia, itakayoadhimishwa Mwezi Oktoba, 2014 mjini Vatican. Wanafamilia wanakumbushwa
kwamba, wamepewa dhamana na wajibu ambao wameuhifadhi katika sahani ya udongo. Familia
ni tabernakulo ya Injili ya Uhai, changamoto kwa wanandoa na familia kujitajirisha
kwa tafakari ya kina ya Neno la Mungu na Maisha ya Kisakramenti. Hiki ni chombo ambacho
kinatumika mara kwa mar ana hivyo kinahitaji uvumilivu unaojikita katika fadhila ya
unyenyekevu, kwani Mwenyezi Mungu amependa kuwateuwa watu wa kawaida ili kuendeleza
kazi ya uumbaji na ukombozi wa mwanadamu. Familia ni chombo ambacho kiko wazi
mbele ya Mungu ili kutekeleza kazi zake na kwamba, thamani na utakatifu wa maisha
ya ndoa na familia vinapata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye muasisi
wa maisha ya ndoa na familia na hivyo kuwekwa katika historia ya ukombozi. Familia
ni hazina inayohifadhi Fumbo la Upendo wa Mungu kwa mwanadamu. Ni hazina inayotishiwa
na utamaduni wa kifo na ukanimungu. Lakini, waamini wakumbuke kwamba, hazina hii bado
inaendelea kulindwa na Mwenyezi Mungu anayehitaji ushirikiano wa wanandoa na familia
pamoja na Kanisa.