Msiwapotoshe watu kwa kuandika habari za uvumi usiokuwa na msingi!
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI amewataka waamini na watu wenye mapenzi mema
kuwapuuza wale wanaoonesha mashaka kuhusu uamuzi wake wa kung'atuka kutoka katika
kiti cha Khalifa wa Mtakatifu Petro. Huu ni uamuzi ambao ameufanya kwa hiyari yake
mwenyewe na kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo.
Haya ni
majibu ambayo yameandikwa kwenye Gazeti "La Stampa" linalochapishwa kila siku nchini
Italia baada ya vyombo kadhaa vya habari ndani na nje ya Italia kuonesha mwelekeo
potofu kuhusu uamuzi wa Baba Mtakatifu Benedikto XVI kung'atuka kutoka madarakani,
takribani mwaka mmoja uliopita, yaani hapo tarehe 11 Februari 2013.
Baba Mtakatifu
mstaafu ameyaandika majibu haya kwa mkono wake mwenyewe, kwa ufupi, lakini kwa usahihi
mkubwa. Anasema huu ni uamuzi ambao ameufanya kwa uhuru na utashi kamili na wala hakuna
shinikizo kutoka sehemu yoyote ile kama ambavyo baadhi ya vyombo vya habari vinataka
kuwaaminisha watu.
Anasema, anaendelea kuvaa mavazi meupe na kutumia jina la
Benedikto wa kumi na sita kwa sababu za kichungaji na wala hakuna mwingiliano wowote
na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro unaoendelezwa na Papa Francisko. Hapa vyombo
vya habari anasema Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI vinataka kupotosha waamini.