Msiogope kupokea Sakramenti ya Mpako wa Wagonjwa ili kukabiliana kwa imani na matumaini
Fumbo la mateso na kifo!
Kwa mpako Mtakatifu wa Wagonjwa na Sala za Makuhani, Kanisa lote huwakabidhi wagonjwa
na wazee kwa Bwana aliyeteswa ba kutukuzwa ili awainue na kuwaokoa. Na kwa hakika,
Kanisa linawahimiza wajiunge kwa hiari na mateso na kifo cha Kristo ili kutoa mchango
wao kwa mafao ya Taifa la Mungu.
Mama Kanisa anapenda kutafakari mang'amuzi
ya ugonjwa na mateso mintarafu huruma ya Mungu inayojionesha kwa Yesu ambaye ni kielelezo
cha Msamaria Mwema. Mama Kanisa kwa kuiga mfano wa Msamaria mwema katika kufundisha
na kuponya kwa njia ya Mpako Mtakatifu wa Wagonjwa."Mtu wa kwenu amekuwa hawezi? Na
awaite wazee wa Kanisa, nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana". Hivi
ndivyo Mama Kanisa ameendelea kutekeleza utume wake kwa wagonjwa kwa njia ya sala
ya Makuhani na Mpako Mtakatifu.
Sakramenti ya Mpako Mtakatifu wa Wagonjwa,
ndiyo mwendelezo wa Katekesi iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe
26 Februari 2014 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Anasema,
kwa njia ya Maadhimisho ya Sakramenti ya Mpako Mtakatifu wa Wagonjwa, Kanisa linawasindikiza
waamini wake ili kukabiliana na Fumbo la Mateso na Kifo.
Baba Mtakatifu anawaalika
waamini na watu wenye mapenzi mema kutambua na kuthamini Sakramenti ya Mpako Mtakatifu
wa Wagonjwa hasa katika tamaduni ambazo zinashindwa kuzungumzia kweli hizi ambazo
zinagusa maisha ya binadamu.
Waamini watambue na kuthamini Sakramenti hii
kama kielelezo cha mshikamano wa maisha ya kiroho na Kanisa zima, kwa kutambua uwepo
endelevu wa Yesu anayewaimarisha wafuasi wake katika imani na matumaini, akiwakumbusha
kwamba, hakuna kitu kinachoweza kuwatenga na nguvu yake inayookoa, si dhambi wala
kifo.
Baba Mtakatifu ametambua uwepo wa wajumbe wa mkutano mkuu wa SIGNIS unaoendelea
mjini Roma. Hiki ni kikundi cha Wanahabari Wakatoliki 300 kutoka katika nchi 80, kinachotafakari
kuhusu "Vyombo vya Habari katika Utamaduni wa amani: kutengeneza taswira na vijana
wa kizazi kipya".
Baba Mtakatifu amewasalimia wanafunzi na marafiki wa Chuo
Kikuu cha Kipapa cha Canada kinachoadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 125 tangu kilipoanzishwa.
Anaendelea kuwahimiza waamini kuhakikisha kwamba, wanapokuwa na mgonjwa au mzee ambaye
yuko katika hatari ya kufa, wasisite kumwita Padre ili aweze kumpatia Mpako Mtakatifu
wa Wagonjwa. Kwa njia hii, Yesu Kristo Mkombozi na Bwana wa maisha, atakuwa karibu
na wagonjwa hawa.
Yesu yupo katika kila Sakramenti ya Kanisa na kwa njia hii
anawashirikisha waamini maisha na huruma yake. Waamini wajitahidi kumfahamu ili hatimaye,
waweze kumhudumia kwa njia ya wagonjwa. Tarehe 27 Februari, Kanisa linafanya kumbu
kumbu ya Mtakatifu Gabrieli mteseka, changamoto kwa vijana kuwa ari na mwamko wa kutaka
kuwa kweli ni wafuasi wa Kristo.
Baba Mtakatifu anawaalika wagonjwa kutolea
shida na mahangaiko yao huku wakijishikamanisha na Kristo. Wanandoa wapya wajitahidi
kuhakikisha kwamba, Injili inakuwa ni dira na mwongozo wa maisha yao.