Maboresho ya uchumi wa Kanisa ni kwa ajili ya mafao na ustawi wa maendeleo ya maskini
na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii
Kardinali George Pell, Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Kipapa ya Uchumi na Fedha anasema,
ikiwa kama Vatican itafanikiwa kuboresha hali yake ya uchumi na fedha, huu utakuwa
ni msaada mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa kwa ajili ya maskini na wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii.
Kardinali Pell kwa miaka kumi na miwili amekuwa ni Askofu
mkuu wa Jimbo kuu la Sydney, Australia kwa sasa anajiandaa kufunga vilago, tayari
kumsaidia Baba Mtakatifu Francisko katika mchakato wa maboresho ya maisha na utume
wa Kanisa mjini Vatican hasa katika masuala ya fedha na uchumi.
Kardinali Pell
anasema kwamba, Sekretarieti ya uchumi itakayosimamiwa na Baraza la Kipapa la Uchumi
itakuwa na dhamana ya kutunga sera, kudhibiti mapato na matumizi ya Vatican na Taasisi
zake. Katika kipindi cha miezi mitatu, Sekretarieti itapembua na kuchambua hali ya
fedha na kuweka bajeti ya kila Baraza la Kipapa na Taasisi za Vatican, kwa kuzingatia
vigezo vya ukweli, uwazi na uwajibikaji. Lengo ni kurahisisha shughuli sanjari na
kuondokana na urasimu usiokuwa na tija.
Baraza la Kipapa la Uchumi litaundwa
na Makardinali wanane na Waamini Walei saba. Kanisa katika masuala ya uchumi na fedha
halina budi kusaidiwa na wataalam waliobobea ili liweze kutekeleza dhamana yake kikamilifu.
Ni matumaini ya Kardinali Pell kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ataweza kumpatia Kikosi
kazi kikamilifu, tayari kuanza kuchapa kazi ambayo kwake imekuwa ni heshima kubwa
kwake. Kanisa halina budi kushirikiana na wataalam pamoja na kutumia wataalam wa uchumi
na fedha kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa.