2014-02-26 09:48:47

Kanisa linatoa kipaumbele cha kwanza kwa Familia katika maisha na utume wake!


Kanisa limeendelea kutoa kipaumbele cha pekee kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kwa kutambua kwamba, Familia ni kitovu cha Uinjilishaji Mpya. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba na tafakari zake anawahimiza wanandoa kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha amani, upendo na mshikamano wa dhati katika hija ya maisha yao ya kila siku.

Anawaalika kutumia maneno ya kawaida tu: Samahani, pole na asante na unihurumie. Familia zinapaswa kujikita katika maisha ya Sala na Tafakari ya Neno la Mungu ili kuimarisha kifungo cha Sakramenti ya Ndoa Takatifu. Bila fadhila hizi, familia nyingi zitajikuta zinageuka kuwa ni uwanja wa fujo na kinzani za kila aina!

Baba Mtakatifu Francisko anatambua fika changamoto zinazoendelea kuzikumba familia nyingi duniani kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa, misimamo na mitazamo tenge juu ya tunu msingi za kijamii na kitamaduni pamoja na ukanimungu; mambo ambayo yamechangia kumong'onyoka kwa tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu.

Licha ya magumu na changamoto zote hizi, lakini watu wengi bado wana hamu na kiu ya kutaka kujenga maisha ya ndoa na familia, kushiriki katika ujenzi wa Jumuiya kwani wanatambua kwamba, kama binadamu wanapaswa kushirikiana na wengine na kwa kuwa wao si kisiwa. Hii ni njia ya kushinda upweke hasi unaoweza kusababisha majanga katika maisha ya mwanadamu.

Kwa bahati mbaya nguvu na ujasiri huu kutoka katika undani wa watu unakumbana na vikwazo na changamoto nyingi kiasi kwamba, baadhi ya watu wanashikwa na kigugumizi cha kufanya maamuzi magumu na mazito katika hija ya maisha yao. Wanaogopa kushikamana na wenzi wao wa ndoa hadi pale kifo kitakapowatenganisha. Hofu hii inarutubishwa na sera na sheria tenge kuhusu maisha ya ndoa na familia, kwa kutafuta mafao binafsi na kusahau wajibu wa kijamii na utu wema. Kimsingi kuna upungufu mkubwa wa sera makini kuhusu tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.

Hii ni tafakari ya kina inayotolewa na Padre Andrea Koprowski, Mkurugenzi wa Vipindi, Radio Vatican anapofanya rejea kuhusu Barua ya Baba Mtakatifu Francisko kwa Ajili ya Familia kama sehemu ya mchakato wa kuzihusisha familia za Kikristo katika maandalizi ya Maadhimisho ya Sinodi Maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia, itakayoadhimishwa mjini Vatican mwezi Oktoba, 2014.

Padre Koprowski anasema watu wengi wana kiu na hamu ya kuwa na familia inayosimikwa katika uhusiano wa dhati kati ya Baba, Mama na Watoto kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu; wanataka kushiriki katika ujenzi wa Jumuiya. Lakini wasi wasi wao mkubwa ni ukosefu wa fursa za ajira; ukosefu wa makazi bora na salama kwa familia zao, wana mashaka ya kufanya maamuzi magumu katika maisha, kwani hawana uhakika na usalama wa kesho kutokana na myumbo wa uchumi kimataifa. Watu kwa sasa wanaishi roho juu juu kama "mkungu wa ndizi".

Kuna makundi ya watu ndani ya Jamii ambayo yamepoteza dira na mwelekeo, hayaoni tena umuhimu wa utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu; hawataki kushiriki katika wito na dhamana ya maisha ya ndoa na familia wala kushiriki katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira ambayo kimsingi ni kazi ya uumbaji. Kundi hili la watu linajikita katika ubinafsi na hali ya kujitafuta lenyewe; ni watu wanaomezwa mno na malimwengu; ni watu ambao wanataka sifa na madaraka; wanataka utajiri wa haraka haraka hata kwa gharama ya maisha ya jirani zao.

Changamoto zote hizi ndizo zilizomsukuma Baba Mtakatifu Francisko kuitisha Sinodi Maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia, kwa Mwaka 2014 ili Mababa wa Sinodi waweze kuchangia kuhusu hali ya maisha ya ndoa na familia katika Majimbo yao; familia mintarafu mwono wa kijamii na kitamaduni pamoja na changamoto zinazoendelea kujitokeza. Sinodi ya Kawaida ya Maaskofu itakayoadhimishwa Mwaka 2015 itaibua mapendekezo ambayo yatapelekwa kwa Baba Mtakatifu ili aweze kuyaundia mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya Kanisa la Kiulimwengu.

Familia ni mada inayopewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu katika Baraza la Makardinali lililohitimishwa hivi karibuni hapa mjini Vatican alisikiliza kwa makini mchango uliotolewa na Makardinali kuhusu tunu msingi za maisha ya ndoa na familia pamoja na changamoto zote. Baba Mtakatifu aliwaambia Makardinali kwamba, Familia ni kiini cha maisha ya Jamii ya binadamu.

Tangu mwanzo, Mwenyezi Mungu aliwaumba mwanamke na mwanaume, ili waweze kuzaa na kuijaza dunia. Tafakari inayofanywa na Mama Kanisa ni kuangalia uzuri wa maisha ya ndoa na familia; kiini cha imani, furaha na matumaini. Kanisa linaangalia machungu na mateso yanayojitokeza katika maisha ya ndoa na familia. Familia leo hii inapuuzwa na kunyanyasika, lakini bado waamini wanatamani kujenga na kudumisha familia kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu.

Kanisa linapenda kuangalia mpango wa Mungu kwa familia ya binadamu, ili kuwasaidia wanandoa na familia kuishi kwa furaha na matumaini makubwa, licha ya magumu na changamoto wanazokabiliana nazo katika hija ya maisha yao hapa duniani. Kumbe si haba anasema Padre Andrea Koprowski, kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ameandika Barua kwa ajili ya Familia za Kikristo kwa kutambua umuhimu wa familia katika maisha na utume wa Kanisa.

Imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.