2014-02-25 12:13:39

Familia ni barua wazi inayopaswa kushuhudia umuhimu wa ndoa na maisha ya kifamilia!


Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Familia anasema, barua iliyoandikwa na Baba Mtakatifu Francisko wahusika wakuu ni Familia za Kikristo zilizoenea sehemu mbali mbali za dunia.

Familia inapewa kipaumbele cha kwanza na Mama Kanisa hasa wakati huu Baba Mtakatifu Francisko anapofanya kumbu kumbu ya Mwaka mmoja tangu alipochaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, tukio linalofuatia baada ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani pamoja na wachumba kukutana na Baba Mtakatifu wakati wa Siku kuu ya wapendanao.

Ndoa na familia ni mada zilizofanyiwa kazi wakati wa mkutano wa Makardinali uliohitimishwa hivi karibuni hapa mjini Vatican kama sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia, itakayoadhimishwa Mwezi Oktoba 2014 hapa mjini Vatican; sanjari na Maadhimisho ya Siku ya Familia Kimataifa itakayofanyika Mwezi Septemba, 2015 mjini Philadelphia pamoja na Sinodi ya kawaida ya Maaskofu kwa ajili ya familia, itakayoadhimishwa mwaka 2015. Haya ni matukio yanayoonesha jinsi ambavyo Mama Kanisa anatoa kipaumbele cha kwanza kwa ajili ya familia ya binadamu na Kikristo kwa namna ya pekee.

Baba Mtakatifu Francisko kwa barua yake kwa familia anapenda kuwaalika wanafamilia kushiriki kikamilifu katika hija na mchakato wa Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa sala kwa kutambua kwamba, familia ndiyo wahusika wakuu kutokana na kifungo cha Sakramenti ya Ndoa. Baba Mtakatifu anaziangalia familia kwa moyo wa shukrani kama kielelezo cha hali ya juu cha upendo wa Mungu unaojionesha kati ya Bwana na Bibi; upendo unaowakumbatia ndugu na jamaa wote.

Tangu mwanzo, Kanisa limekuwa likitoa kipaumbele cha kwanza kwa Familia, kama Maandiko Matakatifu yanavyosimulia. Ndoa kati ya Bwana na Bibi ni Fumbo kubwa kwani lina uhusiano kati ya Kristo na Kanisa lake. Mtakatifu Paulo ameandika vizuri kuhusu muda wa Kanisa, muda wa Familia. Familia za Kikristo zinapaswa kuwajibika katika maisha na utume wake. Anawaomba msaada kutoka kwao, ili familia ziweze kutekeleza wajibu huu msingi kwa kuwajibika katika upendo wao.

Walezi wa maisha ya ndoa na familia wawasaidie wanafamilia kujenga moyo wa sala kwa kumwomba Roho Mtakatifu ili aweze kulisaidia Kanisa kufanya mageuzi yanayokusudiwa. Familia zitambue kwamba, ni wahusika wakuu na kwamba, wao ni barua wazi zinazopaswa kushuhudia zawadi ya maisha ya ndoa na familia si tu kwa maneno, bali kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Familia za Kikristo ziwe ni barua wazi zinazosomwa na watu wengine ili kujifunza matendo makuu ya Mungu yanayogusa undani wa mwanadamu!







All the contents on this site are copyrighted ©.