2014-02-24 08:10:37

Viongozi wa Kanisa wamepewa dhamana ya kuwaongoza watu wa Mungu katika hija ya furaha na utakatifu wa maisha!


Ninyi nyote ni wa Kristo na Kristo ni wa Mungu ni maneno ya Mtakatifu Paulo kwa Wakorintho waliokuwa wamegawanyika na kuwataka kuachana na mawazo hayo potofu kwa kutambua kwamba, Mitume ni sehemu ya Jumuiya ya Waamini na Jumuiya nzima ni mali ya Kristo na wala si vinginevyo.

Majimbo, Parokia pamoja na vyama vyote vya kitume ndani ya Kanisa vina utu na heshima ile ile inayobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo, inayowawezesha wote kujisikia kuwa ni Watoto wa Mungu na ndugu zake Kristo!

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili iliyopita tarehe 23 Februari 2014 mara baada ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na Makardinali kumi na tisa waliosimikwa wakati wa Maadhimisho ya Siku kuu ya Ukulu wa Mtakatifu Petro, Jumamosi iliyopita kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Baba Mtakatifu anasema, wale wote waliopokea daraja kwa ajili ya kuwaongoza watu wa Mungu, kuhubiri pamoja na kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa, watambue kwamba, wamepewa dhamana ya kuwahudumia Watu wa Mungu, kwa kuwasaidia kufanya hija ya furaha na utakatifu wa maisha na kamwe si wamiliki wa dhamana hii kwa ajili ya mafao yao binafsi.

Baba Mtakatifu anasema, Mama Kanisa anawadhaminisha na kuwaalika Makardinali wapya kutolea ushuhuda amini katika maisha na shughuli zao za kichungaji. Ibada ya kuwasimika Makardinali wapya pamoja na adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu, jumapili iliyopita ni matukio yaliyoonesha Ukatoliki wa Kanisa la Kiulimwengu, kwa kuwa na Makardinali wanaowakilisha Makanisa mbali mbali mbali, wote wakimzunguka Khalifa wa Mtakatifu Petro kama kielelezo cha umoja na mshikamano wa Kanisa.

Baba Mtakatifu anawaalika Makardinali kushirikiana naye katika mchakato wa ujenzi wa umoja na mshikamano wa Kanisa kwani umoja ni muhimu zaidi kuliko kinzani na vita kwani umoja ni amri na utashi wa Kristo mwenyewe! Mambo mengine ni mapungufu ya binadamu ambayo kamwe hayapaswi kuendekezwa. Siku mbili za Mkutano wa Baraza la Makardinali imekuwa ni fursa ya kuimarisha: imani, umoja na mapendo kwa Kristo na Kanisa lake.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuendelea kuwasindikiza Makardinali wapya kwa njia ya sala na sadaka zao, ili waweze kutekeleza dhamana kwa Jumuiya iliyokabidhiwa mikononi mwao na Mama Kanisa. Viongozi wa Kanisa wanahitaji kusindikizwa na sala ili kuweza kuwaongoza, kuwatakatifuza na kuwafundisha watu wa Mungu kwa ari na moyo mkuu.

Viongozi wa Kanisa ni wahudumu wa Kanisa na kwamba, familia yote ya Mungu inapaswa kutoa ushuhuda unaoonesha uaminifu wao kwa Kristo na Kanisa lake. Kwa pamoja wafanye hija ya kinabii kwa kutekeleza matamanio ya maisha ya kiroho yanayooneshwa na watu wa nyakati hizi.







All the contents on this site are copyrighted ©.