Rais Rousseff wa Brazil akutana na kuzungumza na Papa Francisko mjini Vatican
Baba Mtakatifu Francisko mwishoni mwa Juma amekutana na kuzungumza na Rais Dilma Rousseff
wa Brazil na ujumbe wake waliokuwa mjini Vatican kushiriki katika Ibada ya kusimikwa
kwa Makardinali wapya, kati yao alikuwepo Kardinali Oran Tempesta, Askofu mkuu wa
Jimbo kuu la Rio de Janeiro, Brazil.
Baba Mtakatifu kwa mara nyingine tena
ametumia fursa hii kwa ajili ya kuwashukuru wananchi wa Brazil kwa moyo wa ukarimu
na upendo waliomwonesha wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka
2013 iliyofanyika nchini Brazil.
Kwa upande wake Rais Rousseff amemwelezea
Baba Mtakatifu Francisko kuhusu maandalizi ya michezo ya Kombe la Dunia kwa Mwaka
2014 itakayofanyika nchini Brazil. Rais amemzawadia Baba Mtakatifu Francisko jezi
ya mpira iliyotiwa mkwaju na "Mchawi wa Kabumbu" Pele kwa heshima ya Baba Mtakatifu
Francisko pamoja na mpira uliotiwa sahihi na Ronaldo. Baba Mtakatifu kwa upande wake
amemzawadia Rais Rousseff medali ya Malaika wa Amani.