Rais Michel Joseph Martelly wa Haiti akutana na kuzungumza na Papa Francisko
Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 24 Februari 2014 amekutana na kuzungumza
na Rais Michel Joseph Martelly wa Haiti pamoja na ujumbe wake, ambao pia walikutana
na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana
na Askofu mkuu Dominique Mamberti, Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano
wa kimataifa mjini Vatican.
Viongozi hawa wawili wameridhishwa na uhusiano
kati ya Haiti na Vatican. Kwa pamoja wamepongeza mchango unaotolewa na Kanisa Katoliki
nchini Haiti. Baba Mtakatifu ni mgeni wake wameonesha haja ya kuendelea kujifunga
kibwebwe kwa ajili ya ujenzi wa Haiti mpya hasa kwa kuimarisha sekta ya elimu na afya
pamoja na huduma za kijamii. Wamekazia pia umuhimu wa majadiliano ya amani kati ya
makundi mbali mbali nchini Haiti ili kujenga upatanisho, umoja wa kitaifa na mafao
ya wengi.