2014-02-24 12:14:18

Miujiza, huruma na upendo wa Kristo ni kielelezo cha Umama wa Kanisa!


Waamini wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, daima wanaambatana na Yesu katika hija ya maisha yao ya kila siku, kwa kutambua kwamba, Yesu mwenyewe yuko kati yao, wakimkimbilia na kumwomba kwa imani na matumaini anaweza kuwakirimia yale wanayohitaji katika maisha yao. Yesu ni mwingi wa huruma na mapendo, jambo linalojionesha katika maisha na utume wake hata pale watu wanapoonesha kuwa na imani haba!

Hayo yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Siku ya Jumatatu, tarehe 24 Februari 2014 wakati wa Ibada ya Misa takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican. Yesu anamhurumia yule Baba aliyekuwa na mtoto aliyepagawa na pepo wachafu, ambao mitume wake hawakuweza kumwondolea. Yesu anamponya na kumrudisha tena nyumbani kwa wazazi wake. Hivi ndivyo alivyofanya alipomfufua rafiki yake Lazaro pamoja na yule Binti wa Yairo.

Yesu alijipambanua kuwa ni mchungaji mwema, alipomtafuta yule Kondoo aliyepotea nyikani kama alivyofanya yule Mwanamke aliyepoteza fedha yake. Hii inaonesha kwamba, Yesu anajali mateso na mahangaiko ya watu wake, ameonesha mshikamano na binadamu anayeteseka, ili kumwelekeza katika hija inayokwenda kwenye nchi ya ahadi. Uponyaji na huruma inayooneshwa na Kristo ni mwaliko kwa kurudi tena Kanisani. Yesu anaponya na kusamehe, kama alivyofanya kwa Mathayo na Zakayo Mtoza ushuru.

Yesu anaendelea kuonesha upendo na ukarimu huu kwa njia ya Kanisa, hakuna mtu anayeweza kumpenda Kristo bila kulipenda Kanisa, kwani Kristo na Kanisa ni chanda na pete! Kila wakati Yesu anapomwita mtu anamwonesha njia inayoelekea kwenye Kanisa, kwani Kanisa ni Mama, mwaliko wa kuendelea kukaa ndani ya Kanisa kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.







All the contents on this site are copyrighted ©.