2014-02-24 09:03:40

Mauaji, uhusiano wa damu na uhusiano ndugu kisheria ni kati ya vizuizi vya ndoa ya Kikristo!


Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, kwa mara nyingine tena karibu katika kipindi chetu cha Kanisa la nyumbani. Katika vipindi vilivyopita tulianza kuvitazama vizuizi vya ndoa kwa sura nyepesi ya Kichungaji. RealAudioMP3

Tunasema tena: Lengo letu, ni kuyapa hadhi, uzuri na heshima kuu zaidi maisha ya ndoa na familia, ili kwamo Mungu atukuzwe na wanadamu watakaswe. Katika kikao chake pamoja na Makardinali, Baba Mtakatifu Francisco katika salaamu zake amewaomba Makardinali wote, kuzamisha mawazo yao katika kuweka mbele ukuu wa Sakramenti ya ndoa na uzuri wa familia.

Hadi sasa tumezungumzia vizuizi saba, yaani umri (kuwa chini ya umri unaokubalika kisheria), uhanithi (kukosa uwezo wa kushiriki tendo la ndoa), ndoa awali, utofauti wa imani, daraja takatifu, nadhiri hadhara ya useja katika Shirika la kitawa na kutoroshwa. Leo mpendwa msikilizaji, tunaendelea...!
Kizuizi cha NANE ni MAUAJI. Sheria Kan, namb. 1090 inakataa ndoa ya mmwagaji damu ili aweze kuoa. Kwa mfano, Ndg. Pori anampenda sana Mwitu. Lakini Mwitu amekwisha kuolewa na Bw. Kichaka. Pori anaamua kumuua Bw. Kichaka ambaye ni mume halali wa Mwitu, ili apate nafasi ya kumuoa Mwitu. Hicho ni kizuizi!

Au mama Ngedere amemchoka kabisa mumewe, badala yake anampenda sana Bw. Nyani na huyu Bw. Nyani yupo tayari kumuoa Mama Ngedere lakini kikwazo ni Bw. Ngedere. Mama Ngedere anaamua kutumia ukatiri wake aliorithi kutoka kwa shetani, anamuua mumewe kwa sumu au kwa kukodi majambazi au kwa kupanga ajali; ili awe huru kuolewa na Bw. Nyani. Au wewe unamuua mchumba wa fulani ili yule fulani akuoe wewe. HICHO NI KIZUIZI. NDOA HIYO ITANUKA DAMU KILA SIKU!!

Kizuizi cha TISA ni UHUSIANO DAMU. Sheria Kan, namb. 1091 inakataza kabisa ndoa kati ya ndugu wa damu daraja la kwanza na daraja la pili hadi ngazi ya nne. Mfano Baba hawezi kumuoa binti yake au mjukuu wake, au dada kuolewa na kaka yake. Pia mtu huwezi kuoa mtoto wa dada yako, au kumuoa dada ya baba yako mzazi. Haitegemewi kusikika kijana unataka kufunga ndoa na mama yako mzazi.

Maingiliano ya kindoa kati ya ndugu wa damu ni tatizo linalokua sana nyakati zetu hizi, kwa sababu za usiri mkubwa na uholela katika uzazi. Kijana na Binti ni watoto wa baba mmoja, ila hawajuani kwa sababu baba aliwazaa sehemu tofauti kwa siri. Taratibu zifuatwe vizuri ili kuona kweli wanaoingia katika agano hawaingii katika uharimu. Uchumba wa kuchunguzwa na matangazo ni kitu muhimu sana. ukisikia ndugu wa damu wanataka kufunga ndoa, ni kizuizi hicho, timua mbio kaseme kwa Paroko.

Kizuizi cha KUMI ni UHUSIANO-NDUGU KISHERIA. Sheria Kan, namb. 1092, tuifafanua kwa mifano zaidi. Maana iliyofichika ni kwamba, kwa kitendo cha kuoa na kuolewa, mume anajenga udugu wa karibu kabisa na ndugu wa mkewe, na mke anajenga udugu wa karibu na ndugu wa mumewe. Ikitokea mmoja anafariki, haitegemewi mama mfiwa aolewe na baba mkwe wake, au baba mfiwa akaoe mama mkwe wake ambaye ni mjane. Au hata ile ambayo hutendeka mahali pengi ya mtu kuamua kuoa mdogo wa marehemu mkewe, au mama anaolewa na mdogo wa marehemu mumewe. Au mtu unaamua tu kukurupua mke wa ndugu yake. Yohane Mbatizaji alimkataza Herode tabia ya aina hiyo. KIMSINGI SIO HALALI. IkitokeA hivyo, usiifiche hali hiyo, taratibu ya kichungaji ifuatwe, Baba Paroko anajua.

Tunaahirisha kipindi chetu kwa leo, tusikilizane tena wakati mwingine. Kutoka Radio Vatican,
Ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.