Madhabahu ya Mashahidi wa Uganda, Namgongo, Uganda kuboreshwa zaidi
Baraza la Maaskofu katoliki Uganda limekamilisha mkakati wa ujenzi wa Hoteli ya Kisasa
itakayo kuwa na ghorofa tatu na vyumba 75 kwenye Madhabahu ya Mashahidi wa Uganda,
Namgongo. Lengo ni kutaka kuboresha huduma kwa mahujaji wanaomiminika kila Mwaka ifikapo
tarehe 3 Juni kwa ajili ya Sherehe ya Mashahidi wa Uganda.
Hayo yamesemwa hivi
karibuni na Askofu mkuu Cyprian Kizito Lwanga wa Jimbo kuu la Kampala wakati wa Maadhimisho
ya Jubilee ya Miaka 135 ya Ukristo nchini Uganda; Ibada ambayo ilifanyika kwenye eneo
la Kigungu, Entebe, Uganda. Madhabahu ya Mashahidi wa Uganda, Namgongo kimekuwa ni
kivutio kikubwa cha mahujaji kutoka sehemu mbali mbali ndani na nje ya Uganda wanaokwenda
kushuhudia mahali ambapo Mashahidi wa Uganda waliweza kuyamimina maisha yao kwa kuthubutu
kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake dhidi ya madhulumu na nyanyaso zilizotolewa
na Mfalme Kabaka Mwanga wa, kwenye miaka 1880.
Ujenzi wa Hoteli hii inakadiriwa
kugharimu kiasi cha Shilingi za Uganda billioni 2.5 hadi utakapokamilika. Hoteli iliyopo
kwa sasa itaboreshwa zaidi ili kukidhi viwango vya kimataifa. Askofu mkuu Lwanga anasema,
mradi huu ni sehemu ya vitega uchumi vya Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Uganda.