2014-02-24 07:40:00

Maaskofu wa Hispania waanza hija ya kitume mjini Vatican


Kundi la kwanza la Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania, tarehe 24 Februari 2014 linaanza hija ya kitume inayofanyika mjini Vatican walau kila baada ya miaka mitano kadiri ya sheria za Kanisa. Kundi la kwanza linaundwa na Maaskofu 44, litapata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu pamoja na viongozi waandamizi kutoka Vatican. RealAudioMP3

Taarifa zinaonesha kwamba, kundi la pili litakutana na Baba Mtakatiofu Francisko kuanzia tarehe 3 hadi tarehe 8 Machi 2014. Baba Mtakatifu anatarajiwa kukutana na Maaskofu wote wa Hispania hapo tarehe 3 Machi 2014. Kwa mara ya mwisho, Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania lilifanya hija yake ya kichungaji kunako mwaka 2005. Hata kama walihitimisha hija yao kadiri ya sheria za Kanisa, lakini hali ya Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili iliendelea kudhohofu sana.

Katika uongozi wa Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI, Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania halikupata nafasi ya kufanya hija ya kitume mjini Vatican. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI alibahatika kutembelea Hispania mara tatu wakati wa utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Mara ya kwanza ilikuwa ni Mwaka 2006 wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Tano ya Familia Kimataifa iliyoadhimishwa mjini Valencia. Kunako mwaka 2010 Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alitembelea mjini Barcelona na Santiago de Compostella.

Vijana wengi wanaikumbuka hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI mjini Madrid wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2011, wakati vijana waliponyeeshewa na mvua kubwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto akabaki pamoja nao! Adhimisho likaendelea kama ilivyopangwa kwa Kesha na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu.








All the contents on this site are copyrighted ©.