Harambee ya kununua vifaa tiba kwa ajili ya wodi ya Watoto, Hospitali ya Muhimbili
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete Jumamosi, Februari
22, 2014, aliongoza harambee ya kupatikana kwa zaidi ya sh milioni 600 kwa ajili ya
ununuzi wa vifaa vya kisasa vya matibabu kwa ajili ya Wodi ya Watoto katika Hospitali
ya Taifa, Muhimbili, Dar Es Salaam.
Katika halfa hiyo iliyofanyika kwenye Hoteli
ya Golden Tulip, Dar Es Salaam, Rais Kikwete pia ameahidi kuendeleza kuongoza jitihada
za kupatikana kwa kiasi cha sh milioni 328 ambazo zinahitaji kukamilisha hesabu ya
sh. 929, 915,000 ambazo ndizo zilikuwa lengo la halfa hiyo.
Halfa hiyo pia
iliwakutanisha viongozi wakuu wa awamu tatu za uongozi wa juu wa Tanzania ambako Rais
wa Pili wa Tanzania, Mzee Ali Hassan Mwinyi na Rais wa Tatu za Tanzania, Mzee Benjamin
William Mkapa walikuwa wenyeji wa halfa hiyo kwa nyadhifa zao kama walezi wa Chama
cha Madaktari wa Watoto Tanzania (PAT).
Uchangiaji katika halfa hiyo ulikuwa
wa aina tatu – kuna fedha taslimu milioni 55.4 zilizochangwa moja kwa moja, kuna ahadi
za uchangiaji na kuna wachangiaji walioamua kuwa watatoa fedha za kununua vifaa mbali
mbali vinavyohitajika katika Wodi hiyo ambayo gharama yake inakadiriwa kufikia dola
za Marekani 570,500.
Katika halfa hiyo, Ikulu ya Rais Kikwete imetoa mchango
wa kununua mashine iitwayo “Infant Radiant Warmer” yenye thamani ya dola za Marekani
15,300 wakati Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) inayoongozwa na Mama Salma Kikwete
imechangia ununuzi wa mashine iitwayo Compressor Nebulizer ambayo gharama yake ni
dola za Marekani 12,000.