2014-02-24 09:59:31

Balozi Fulgence Kazaura, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amefariki dunia!


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ameelezea mshituko na masikitiko yake kufuatia kifo cha Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar Es salaam (UDSM), Balozi Fulgence Kazaura kilichotokea nchini India, Jumamosi, Februari 22, 2014.

Katika salamu zake za rambirambi kwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mheshimiwa Dkt. Shukuru Kawambwa, Rais Kikwete amesema: “Nimepokea kwa mshituko, masikitiko na huzuni taarifa ya kifo cha Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Balozi Flugence Kazaura, ambacho nimejulishwa kuwa kimetokea katika Kituo cha Matibabu ya Kansa katika mji wa Chennai, nchini India.”

“Kwa hakika, kifo cha Mzee Kazaura siyo kwamba kimekipokonya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kiongozi hodari na mwenye visheni kubwa, lakini kifo hicho kimeondolea Tanzania mmoja wa watumishi hodari wa umma. Mzee Kazaura pia alikuwa mtumishi mwaminifu na mwadilifu kwa nchi yake na sote tunaendelea kwa kumkumbuka kwa sifa hizo na mchango wake mkubwa katika utumishi wa umma,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:

“Alithibitisha sifa hizo katika nafasi zote alizozishikilia katika maisha yake tokea alipokuwa Katibu Mkuu katika wizara mbali, hadi alipokuwa Balozi wa Tanzania Makao Makuu ya Umoja wa Ulaya (EU) na nchini Ubelgiji, hadi alipoteuliwa Mshauri Maalum wa Uchumi wa Rais, hadi alipokuwa Naibu Katibu Mkuu wa Jumuia ya Afrika Mashairiki (EAC) katika uongozi mbali mbali za Bodi za mashirika ya umma na binafsi na hata kwenye nafasi yake ya Ukuu wa Chuo Kikuu cha Dar Es salaam kwa miaka tisa. Tutaendelea kumkumbuka.”

Ameongeza Rais Kikwete: “Nakutumia wewe Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dkt. Shukuru Kawambwa salamu zangu za rambirambi kufuatia msiba huu mkubwa. Aidha, kupitia kwako naitumia jumuia nzima ya Chuo Kikuu cha Dar Es Salaam pole nyingi kwa kuondokewa na kiongozi wao.”

“Nakuomba pia unifikisshie salamu zangu za pole nyingi kwa familia ya Mzee Kazaura. Wajulishe kuwa naungana nao katika kuomboleza kifo cha Mzee wetu huyu na kwamba msiba wao ni msiba wangu pia. Pia naomba wajue kuwa naungana nao katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke mahali pema peponi roho ya Marehemu Fulgence Kazaura. Amina.”


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameihakikishia Misri kuwa Tanzania itaunga mkono jitihada za nchi hiyo kurejeshewa uanachama wake katika Umoja wa Afrika (AU) baada ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa kidemokrasia nchini humo Aprili mwaka huu.

Rais Kikwete pia amesisitiza kuwa msimamo wa Tanzania kuhusu matumizi ya maji ya Mto Nile ni kwamba nchi zote ambako Mto huo unapitia, kwa namna moja ama nyingine, zina haki sawa ya kutumia maji ya Mto huo kwa maendeleo ya nchi hizo. Aidha, Rais Kikwete ameishukuru Misri kwa kuchangia maendeleo ya Tanzania kwa kuunga mkono jitihada hizo kwa misaada katika sekta mbali mbali na hasa sekta za maji na afya.

Rais Kikwete ameyasema hayo jioni, Jumamosi, Februari 22, 2014, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, Mheshimiwa Nabil Fahmy ambaye pia amewasilisha ujumbe maalum kwa Rais Kikwete kutoka kwa Rais wa muda wa Misri, Mheshimiwa Adly Mansour.

Katika mazungumzo hayo, Mheshimiwa Fahmy aliiomba Tanzania kuunga mkono jitihada za Misri kurejeshewa uanachama wake wa AU kufuatia kusikitishwa kwa uanachama huo baada ya kuondolewa madarakani kwa kiongozi wa nchi hiyo aliyekuwa amechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia, Mheshimiwa Mohamed Morsi mwaka jana.

Rais Kikwete alimhakikishia Waziri Fahmy kuwa Tanzania haitasita kuunga mkono jitihada hizo lakini baada ya Misri kuwa imefanya uchaguzi wa kidemokrasia mwezi Aprili mwaka huu. “Kwa mujibu wa Makubaliano ya Uanzishwaji wa AU, itakuwa vigumu kwa Misri kurejeshewa uanachama wake katika mazingira ya sasa. Lakini baada ya kuwa kufanyika kwa uchaguzi wa kidemokrasia kuchagua kiongozi mpya, Tanzania itakuwepo kuunga mkono jitihada hizo za Misri,” Rais kikwete alimwambia Waziri Fahmy.

Kuhusu matumizi ya maji ya Mto Nile, Rais Kikwete alisisitiza msimamo wa Tanzania wa kuwa ni haki ya kila nchi ambako Mto huo unapitia kutumia maji yake kwa maendeleo yake. “Tunaamini katika Haki ya Matumizi ya Maji kwa nchi zote ambako Mto huu unapitia. Ni aina ya haki hiyo ambayo inatumika hata Tanzania kulingana na matumizi ya maji ya mito mbali mbali ndani ya Tanzania,”

Mapema Waziri Fahmy alimwambia Rais Kikwete kuhusu umuhimu wa maji ya Mto Nile kwa nchi ya Misri akisema: “Sisi katika Misri hupata mvua kwa siku tatu kwa wastani kwa mwaka. Maji yote tunayotumia yanatokana na Mto Nile. Hivyo, unaweza kuelewa umuhimu wa Mto huo kwa uhaki na ustawi wa nchi yetu.” Rais Kikwete pia ameishukuru Misri kwa misaada yake ya maendeleo kwa Tanzania hasa katika sekta za afya na maji.








All the contents on this site are copyrighted ©.