2014-02-22 11:48:35

Papa ateuwa Marais watakaosimamia Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu Familia


Baba Mtakatifu Francisko amemshukuru na kumpongeza Kardinali Walter Kasper aliyewawezesha Mababa wa Kanisa kufanya tafakari ya kina kuhusu umuhimu wa familia kadiri ya mpango wa Mungu pamoja na kuangalia changamoto zinazoendelea kujitokeza katika maisha ya ndoa na familia, ili Kanisa liweze kuibua mbinu mkakati wa kichungaji utakaowawezesha waamini kuendelea kutambua umuhimu wa familia katika maisha na utume wa Kanisa na Jamii katika ujumla wake.

Baba Mtakatifu amemwambia Kardinali Kasper kwamba, tafakari yake ni taalimungu iliyoandikwa kwa njia ya kupiga magoti. Baba Mtakatifu amewateua Makardinali Andrè Vingt-Trois, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Paris, Ufaransa, Kardinali Raymundo Damascene Assis kutoka Brazil pamoja na Kardinali Luis Antonio Tagle kuwa ni Marais wateule wakati wa Maadhimisho ya Sinodi Maalum ya Maaskofu kuhusu Familia itakayofanyika mjini Vatican mwezi Oktoba, 2014. Majina haya yametajwa na Baba Mtakatifu Francisko mbele ya Makardinali 150 waliokuwa wanahudhuria Mkutano wa Makardinali kuhusu Familia hapa mjini Vatican.

Makardinali hawa watasaidiana na Kardinali Peter Erdo na Askofu mkuu Bruno Forte walioteuliwa na Papa Francisko kuwa wahamasishaji wakuu wakati wa Maadhimisho ya Sinodi Maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia. Makardinali wengi waliweza kuchangia katika mada kuhusu Familia na wengine wametoa mchango wao kwa njia ya maandishi na utazingatiwa. Makardinali wameangalia familia ya binadamu mintarafu mafundisho ya Kanisa; mahusiano ya kibinadamu mintarafu mpango wa Mungu; madhara ya utandawazi na mwelekeo potofu wa maisha ya ndoa na familia.

Mafundisho ya Kanisa kuhusu ndoa na familia yamejikita katika mchango uliotolewa na Mwenyeheri Yohane Paulo II katika Waraka wake wa Kichungaji, Familiaris Consortio yaani "Wajibu wa Familia za Kikristo katika Ulimwengu Mamboleo" pamoja na Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki. Makardinali wamedodosa baadhi ya mikakati ya kichungaji kwa ajili ya maisha ya ndoa na familia; umuhimu wa maandalizi makini kwa wanandoa; tasaufi ya maisha ya ndoa na familia.

Mababa wa Kanisa wamegusia pia tatizo la wanandoa waliooana wakaachana na baadaye kuoa au kuolewa tena mintarafu sheria za Kanisa kuhusu uhalali wa ndoa na sababu zinazoweza kupelekea kufutwa kwa ndoa zilizofungwa Kanisani. Padre Federico Lombardi anasema, majadiliano yote haya yamefanyika katika hali ya utulivu pamoja na kuangalia uwezekano kwa waamini wenye shida na mahangaiko haya kupewa Sakramenti za Kanisa kwa kuangalia: huruma ya Kristo, uaminifu kwa Kristo na Kanisa lake na kwamba, haya ni mambo yanayopaswa kuangaliwa kwa watu husika.

Mawazo yote haya ni sehemu ya hija ya Maadhimisho ya Sinodi ya Maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia. Tafakari hizi zimejikita katika Neno la Mungu na Mafundisho ya Kanisa. Familia za wakimbizi na wahamiaji pamoja na familia za Kikristo zinazoishi katika nchi ambazo zinajikuta zina idadi ndogo ya Wakristo.







All the contents on this site are copyrighted ©.