Mababa wa Kanisa waguswa na mahangaiko ya watu kutokana na vita na madhulumu na nyanyaso
za kidini!
Baraza la Makardinali katika mkutano wake wa kawaida uliokuwa chini ya uongozi wa
Baba Mtakatifu Francisko, lilipata nafasi ya kufanya tafakari ya kina kuhusu umuhimu
wa familia kadiri ya mpango wa Mungu na changamoto zake katika ulimwengu mamboleo.
Baba Mtakatifu na Makardinali waliguswa pia na vita na kinzani za kijamii zinazoendelea
kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia, kiasi cha kutuma ujumbe wa mshikamano na upendo
kwa Maaskofu mahalia nchini Ukrain.
Mababa wa Kanisa waliwakumbuka pia watu
wanaoteseka kutokana na vita pamoja na mashambulizi ya kigaidi, hali ambayo kwa sasa
inaonekana kuwa ni jambo la kawaida kwa baadhi ya watu. Maeneo haya ni Nigeria, Sudani
ya Kusini, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati na Syria. Akizungumzia kuhusu matukio
haya, Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, vurugu
na matukio yote haya yanahatarisha amani na utulivu miongoni mwa Jamii.
Baba
Mtakatifu pamoja na Makardinali wametolea sala kwa ajili ya Wakristo sehemu mbali
mbali za dunia wanaoteseka na kudhulumiwa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa
lake. Wakristo wanaendelea kuhimizwa kuwa imara katika imani pamoja na kuwasamehe
watesi na wote wanaowadhulumu, huku wakijitahidi kumuiga Yesu mwenyewe aliyethubutu
kuwasamehe watesi wake kwani walikuwa hawajui wanalotenda!
Ni matumaini ya
Mababa wa Kanisa kwamba, Jumuiya ya Kimataifa itaendelea kujielekeza zaidi katika
kusaidia mchakato wa haki, amani, utulivu, umoja na mshikamano wa kitaifa; kwa kukuza
na kudumisha utawala wa sheria na demokrasia ya kweli. Kinzani na migogoro mingi inayoendelea
kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia ina mwelekeo wa kidini, hali ambayo baadhi
ya watu wanaweza kudhani kwamba, ni vita kati ya Wakristo na Waislam, na kusahau kwamba,
haya ni mambo yanayojikita katika: uchu wa mali na madaraka; ukabila usiokuwa na tija
wala mashiko; umaskini na hali ngumu ya maisha.
Kanisa Katoliki linalaani na
kushutumu vita yoyote ile inayofanywa kwa msingi wa kidini na kwamba, litaendelea
kujielekeza zaidi na zaidi katika mchakato wa kutafuta, kudumisha na kuenzi: haki,
amani na upatanisho kwa ajili ya mafao ya wengi. Kanisa linaendelea kuwahimiza waamini
na watu wote wenye mapenzi mema, kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini
na kiekumene, pamoja na kuonesha ushuhuda wa imani tendaji kwa njia ya matendo ya
huruma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.