Katiba Mpya ya Zambia iwe ni sehemu ya matunda ya Jubilee ya Miaka 50 ya Uhuru nchini
Zambia!
Jubilee ya Miaka 50 ya Uhuru wa Zambia, iwe ni fursa kwa wananchi kujipatia maendeleo
makubwa zaidi kwa kuondokana na umaskini wa hali na kipato; magonjwa pamoja na ukosefu
wa haki msingi za binadamu. Hii ndiyo changamoto inayotolewa na Jukwaa la Viongozi
wa Kikristo nchini Zambia lijulikanalo kama "Oasis Forum" wakati huu Zambia inapojiandaa
kuadhimisha Jubilee ya Miaka 50 tangu ilipojipatia uhuru wa bendera.
Jukwaa
la Viongozi wa Kikristo linasema, inasikitisha kuona kwamba, Zambia inaadhimisha Jubilee
ya Miaka 50 ya Uhuru wa Bendera wakati ambapo kuna umati mkubwa wa wananchi unaoendelea
kuogelea katika dimbwi la umaskini, njaa na ujinga, kiasi hata cha kutishiwa usalama
wa maisha na viongozi waliowachagua na kuwapatia madaraka.
Jukwaa la Viongozi
wa Kikristo linawapongeza wananchi wote wa Zambia waliojifunga kibwebwe wakapigania
na hatimaye wakapata Uhuru wa Bendera. Ni kundi la wananchi wa Zambia lililokuwa na
mtazamo mpana, vipeo na utume uliotakiwa kutekelezwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo
ya wananchi wote wa Zambia.
Wazambia walitamani kujenga na kuendeleza uhuru
na demokrasia si tu kwa kujitawala kutoka katika makucha ya wakoloni bali pia walitaka
kuhakikisha kwamba, wananchi wa Zambia kwa njia ya mshikamano wa upendo na umoja wa
kitaifa wangeweza kuupatia kisogo umaskini, njaa na maradhi; tayari kusimama kidete
kupinga ukosefu wa haki msingi za binadamu na unyonywaji unaoweza kuendelezwa kwa
kuwatumia viongozi wa ndani.
Jukwaa la viongozi wa Kikristo linasema, njia
makini na murua kabisa ya kuwaenzi wapigania uhuru kutoka Zambia katika Maadhimisho
ya Jubilee ya Miaka 50 ya Uhuru wa Bendera ni kuhakikisha kwamba, Katiba Mpya ya Zambia
inapatikana kwa muda muafaka, ili Zambia iweze kufikia malengo, vipeo na utume wake
kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wake.
Kimsingi Jukwaa la viongozi
wa Kikristo halipingi Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 50 ya Uhuru wa Bendera nchini
Zambia, bali linachotaka ni kuhakikisha kwamba, kumbu kumbu hii inaacha alama ya kudumu
kwa wananchi wa Zambia katika harakati na mchakato wa kukuza na kudumisha demokrasia,
utawala wa sheria, ustawi na mafao ya wengi.