2014-02-21 10:00:24

Vyama vya kiraia vina mchango mkubwa katika mchakato wa kutafuta amani, umoja na utulivu Sudan ya Kusini


Askofu mkuu Daniel Balvo, Balozi wa Vatican nchini Sudan ya Kusini na Kenya katika mahojiano maalum na Shirika la Habari za Afrika, CISA anasema, ili amani ya kudumu iweze kupatikana nchini Sudan ya Kusini, kuna haja kwa Serikali kuhakikisha kwamba, inavishirikisha vyama vya kiraia katika mchakato wa kutafuta amani.

Kanisa kwa miaka mingi limekuwa ni mdau mkubwa wa majadiliano ya haki, amani na upatanisho nchini Sudan, linatekeleza dhamana hii kwa ajili ya mafao ya wengi, ndiyo maana linawataka wahusika wakuu wa vita nchini Sudan ya Kusini kusitisha vita na kujikita zaidi katika majadiliano ya amani. Waathirika wakuu wa vita inayoendelea nchini Sudan ya Kusini ni raia wasiokuwa na hatia.

Nchi ya Sudan ya Kusini imebahatika kuwa na rasilimali nyingi ambazo zinaweza kutumika kwa ajili ya kusaidia mchakato wa maendeleo endelevu ya wananchi wa Sudan ya Kusini, lakini jambo hili linawezekana tu, ikiwa kama amani na utulivu vitapewa kipaumbele cha kwanza.

Vatican itaendelea kuchangia pia ustawi na maendeleo ya wananchi wa Sudan ya Kusini pamoja na kusaidia upatikanaji wa: haki, amani na utulivu mambo msingi yanayoweza kukoleza maendeleo ya kweli. Ni vigumu kukoleza maendeleo ya watu ambao wanang'angania vita kama suluhu ya ufumbuzi wa matatizo na changamoto zinazowakabili.

Uchu wa mali na madaraka ndicho kiini cha vita, kinzani na migogoro ya kijamii inayoendelea Sudan ya Kusini. Licha ya wahusika wakuu kukubaliana kusitisha vita lakini bado mapambano ya silaha yanaendelea nchini Sudan ya Kusini.

Askofu mkuu Daniel Balvo amewataka pia wananchi wa Kenya kujenga na kudumisha upendo, umoja na mshikamano wa kitaifa ili kukabiliana fika na mashambulizi ya kigaidi yanayoendelea kujitokeza hasa Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi.







All the contents on this site are copyrighted ©.