2014-02-21 08:41:42

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Saba ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa


Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican kipindi tafakari masomo Dominika, ninakuletea ujumbe wa Neno la Mungu nikisema kuweni watakatifu kama Baba yenu aliye mbinguni. Huo ndo wito wa kila awaye yote anayetaka kupata wokovu yaani uzima wa milele. Tuko tayari Dominika ya VII ya mwaka A wa Kanisa. RealAudioMP3
Katika Somo la kwanza kutoka Kitabu cha Mambo ya Walawi, tunapata kuanza kusikia mwaliko wa kuwa watakatifu tukifuata mfano thabiti na wa uhakika yaani Mungu mwenyewe. Mungu anawasiliana na taifa lake kwa njia ya Musa akitaka wawe watakatifu kama yeye alivyo. Anasonga mbele akieleza kilichomo ndani ya safari ya utakatifu: kuachana na chuki, kukemea maovu yanayojiri katika jumuiya na majirani zetu na kuachana na kinyongo na kisirani katika maisha yako. Ili kutekeleza haya lazima kujitenga na dunia, kama iliyo maana ya utakatifu katika Agano la Kale (mkumbuke Mtakatifu Antonio Abate, mwanzilishi wa Umonaki).

Kwa hakika utakatifu ulikuwa na maana ya kuwekwa pembeni kwa ajili ya Mungu. Patakatifu pa patakatifu palimaanisha Mungu mwenyewe. Ni katika maana ileile, wakristu lazima wajitenga kiroho na chachu ya dunia yaani kuachana na maisha ya dhambi. Ndiyo kusema kukazia amri ya mapendo kwa jirani na si kujitenga na wapagani kama Waisraeli walivyokuwa wakifikiri. Ni kumpenda Mungu tukiambatana na wenye shida mbalimbali tukielekea wote mbinguni.

Mtume Paulo anapowaandikia Wakorinto anakazia ule utakatifu tuliokabidhiwa na Mungu. Anasema sisi ni hekalu la Roho Mtakatifu. Mpendwa msikilizaji, nikishasikia neno hilo mara moja mwaliko ni kutunza utakatifu ili niendelee kubaki Hekalu safi kwa ajili ya kumwabudia Mungu. Katika Ukorinto kulikuwa na ugomvi na ulitokana na tishio la kutopendana na hapa ndipo Mtume Paulo anakuja na fundisho kali akikemea uozo huo unaojitokeza katika sura ya utengano.

Katika Injili, Mwinjili Matayo, anaweka mbele yetu mausia ya Bwana kuhusu sheria ya kale. Bwana anataka mabadiliko ya uelewa wa sheria, yakwamba ni kwa ajili ya kujenga umoja kwa watu na si kuangamiza. Anataka sheria izame katika utu zaidi kuliko mambo mengine na ilinde maisha, iliyo zawadi ya Mungu. Mpendwa mwanatafakari, Hata hivyo yatupasa kuelewa nini maana ya sheria za zamani, mfano Jicho kwa jicho au jino kwa jino!! Mara kadhaa tunatafsiri jambo hili kadiri ya maneno yalivyo kwa nje! Na hivi huleta maana potofu! Kwa hakika mwanzo wa sheria hii ulikuwa mzuri!

Maana yake nini! Ni kwamba kabla ya sheria hii mtu alipokuwa akitenda kosa fulani alikuwa analazimika kulipa fidia si kwa makosa yake tu bali hata kwa makosa mengine yasiyo yake. Na hivi ikawa ni mateso makubwa kwa watu, basi ikatungwa sheria ya jicho kwa jicho, yaani mtu alipie fidia ya makosa yake tu! Kumbe kukazaliwa namna mpya na ya haki katika kutawala na kuongoza haki katika JUMUIYA. Ndiyo kusema hakukuwa na matumizi ya moja kwa moja yaani ya kuondoana macho au meno! Ndiyo kusema walitaka kufundisha ule uwiano kati ya kosa na adhabu .

Mpendwa msikilizaji, Bwana anasema imeandikwa jicho kwa jicho kama njia ya kutenda, lakini mimi nasema epukeni magomvi, majibizano katika maisha yenu. Ni heri kuvumilia na kuachana na mwendelezo wa mapigano. Hataki kuondoa haki ila anataka kuwepo na upole na unyenyekevu wa moyo katika maisha ya watu wakitafuta haki, ili mbele ya taabu tupate kutunza umoja na utulivu katika jumuiya.

Bwana anafundisha kwa hakika, njia ya pekee ya kuondoa mnyololo wa fitina ni msamaha. Kwa maana mtu akikupiga na ukamsamehe mara moja hakuna nyongeza ya ukubwa wa mapigano, lakini kama ukijibu kwa mapigano basi nyongeza mara mbili ya shida katika jumuiya. Anazidi kukazia upendo hata kwa adui, na hii ndiyo namna ya kwenda kinyume na mantiki ya zamani kuhusu upendo.

Mpendwa, mantiki ya zamani na ya sasa kuhusu upendo ni ipi? Kwa hakika hapo zamani ilikuwa mpende akupendaye kinyume na mantiki ya Kristu katika Agano Jipya isemayo, mpende hata adui yako. Bwana haondoi ile ya kwanza bali anaiongezea nguvu na kuikamilisha. Mpendwa, yashike haya yote yaliyousiwa na Bwana na kuyaishi na hivi utakuwa mtakatifu kama Baba yetu aliye mbinguni.

Nikutakie furaha na matumaini katika kuishi sheria mpya, sheria ya Mungu itujengeayo uhuru na mshikamano na Kristo. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.