2014-02-21 09:13:46

Kanisa Katoliki nchini Haiti linamshukuru Papa Francisko kwa kuwaamini na kuwajengea matumaini!


Baraza la Maaskofu Katoliki Haiti linasema kwamba, Mwaka 2014 ni Mwaka wa Neema na Baraka kwani wanasherehekea Miaka 210 tangu Haiti ilipojipatia uhuru wake. Kanisa Katoliki nchini Haiti linaungana na waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa ajili ya Kardinali mteule Chibly Langlois, Askofu wa Jimbo Katoliki Cayes na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Haiti.

Askofu Langlois anakuwa ni Kardinali wa kwanza kuwahi kuteuliwa kutoka Haiti, kumbe, hii ni sehemu ya furaha kwa wananchi wa Haiti na Kanisa katika ujumla wake. Baraza la Maaskofu Katoliki Haiti linapenda kuchukua nafasi hii kwa namna ya pekee kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwaona na kuonesha imani kubwa kwa wananchi wa Haiti ambao pia wanaweza kuchangia katika maendeleo na ustawi wa Kanisa la Kiulimwengu kwa njia ya ushauri kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Maaskofu wanasema, hiki ni kipindi cha matumaini na majadiliano ya kina yanayosimikwa katika ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa Haiti. Maaskofu wanapenda kuwa n chachu ya majadiliano katika mchakato wa kutafuta suluhu ya kudumu kwa kinzani na migogoro inayoendelea kuwakumba wananchi wa Haiti.

Maaskofu wanawasindikiza wanasiasa katika kipindi hiki kigumu kwa njia ya sala na tafakari ili yote yafanyike kwa ajili ya ustawi na mafao ya wananchi wengi nchini Haiti. Baraza la Maaskofu Katoliki Haiti linasema, hapo tarehe 9 Machi 2014 litaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa kumpata Kardinali wa kwanza kutoka Haiti.

Ibada hii ya Misa Takatifu itafanyika kwenye Uwanja wa michezo Syvio Cator mjini Port Prince. Tarehe 7 Februari 2014, Baraza la Maaskofu liliwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kufunga na kusali ili kusaidia mchakato wa majadiliano, amani, upatanisho wa kitaifa na mafao na maendeleo ya wengi: kiroho na kimwili.








All the contents on this site are copyrighted ©.