Askofu mteule wa Jimbo Katoliki Monze, Zambia anatarajiwa kuwekwa wakfu na kusimikwa
rasmi hapo tarehe 3 Mei 2014
Askofu mteule Moses Hamungole wa Jimbo Katoliki Monze, Zambia aliyeteuliwa hivi karibuni
na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu Mpya wa Jimbo Katoliki Monze, Jumatano tarehe
19 Februari 2014 alikiri kanuni ya Imani na kula kiapo cha utii kwa Khalifa wa Mtakatifu
Petro, katika Ibada iliyofanyika kwenye Kikanisa cha Baraza la Kipapa la uenezaji
wa imani. Askofu mteule Hamungole anatarajiwa kuwekwa wakfu na kusimikwa rasmi kuwa
Askofu wa Jimbo Katoliki Monze hapo tarehe 3 Mei 2014
Ibada hii
imehudhuriwa na viongozi waandamizi kutoka Baraza la Kipapa la Uenezaji wa Imani,
wananchi wa Zambia, wafanyakazi kutoka Radio Vatican pamoja na marafiki. Lengo la
Ibada hii ni kumkumbusha Askofu mteule kwamba, baada ya kuteuliwa na Baba Mtakatifu
kuongoza, kuwatakatifuza na kuwafundisha Watu wa Mungu Jimbo Katoliki la Monze sasa
anakuwa ni chombo cha neema kwa watu wake na hivyo atapaswa kumtegemea Mwenyezi Mungu
katika maisha na utume wake, daima akijitahidi kuwa mwaminifu kwa Kristo na Kanisa
lake.
Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mwambata na Rais wa Mashirika ya
Kimissionari ya Kipapa, alimtakia kheri na baraka kwa utume huu mpya. Anaialika Familia
ya Mungu Jimbo Katoliki Monze kumwonesha umoja, ushirikiano na mshikamano Askofu mteule
Moses Hamungole katika maisha na utume wake kama Askofu wa Jimbo Katoliki Monze.