Mahubiri ya Papa Francisko wakati wa Misa za asubuhi, yako mitaani!
Kitengo cha uchapaji cha Vatican, LEV, kimechapisha Kitabu cha Pili cha Mahubiri ya
Baba Mtakatifu Francisko anayotoa kila siku wakati wa Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi
Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican. Hizi ni Ibada
zinazohudhuriwa na makundi mbali mbali ya waamini kutoka ndani na nje ya Vatican.
Kitabu hiki cha Pili ni mkusanyiko wa Mahubiri ya Baba Mtakatifu Francisko
kuanzia tarehe 2 Septemba 2013 hadi kufikia tarehe 31 Januari 2014. Kitabu hiki kwa
sasa kinapatikana katika lugha ya Kiitalia na tafsiri yake kwa lugha ya Kiingereza
iko mbioni kutolewa ili kutoa nafasi kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kuendelea
kufanya tafakari ya Neno la Mungu kadiri ya mawazo na changamoto inayotolewa na Baba
Mtakatifu Francisko.
Kitabu hiki ni mfululizo wa Vitabu vingine sita vilivyoandikwa
kuhusiana na mahubiri na hotuba za Baba Mtakatifu Francisko. Baadhi ya vitabu hivi
ni "Maneno ya Papa Francisko" "Niombeeeni" "Usipokonywe matumaini", "Injili ya Furaha"
Inapendeza sisi kuwepo hapa" "Mahubiri ya Papa Francisko" na "Tembeeni katika njia
ya amani".