Jinamizi la vikwazo vya kiuchumi bado linamwandama Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe
Mawaziri wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa Umoja wa Ulaya wameiondolea
Zimbabwe vikwazo vya kiuchumi, lakini wamekataa kumwondolea vikwazo hivyo Rais Robert
Mugabe wa Zimbabwe. Hivi ni vikwazo ambavyo Zimbabwe iliwekewa kunako mwaka 2002 wakati
wa machafuko ya hali ya kisiasa yaliyopelekea kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Uvunjwaji
wa haki msingi za binadamu na kuchechea kwa mfumo wa demokrasi nchi Zimbabwe ni kati
ya mambo msingi yaliyopelekea Umoja wa Ulaya kuiwekea Zimbabwe vikwazo vya kiuchumi.
Kutokana na vikwazo hivi, Rais Robert Mugabe hataruhusiwa kusafiri katika nchi za
Ulaya hadi tarehe 20 Februari 2015 vikwazo hivi vitakapokwisha muda wake.
Rais
Mugabe hapo tarehe 21 Februari 2014 atasherehekea Miaka 90 tangu alipozaliwa na miaka
34 ya kuiongoza Zimbabwe kama Rais, bado anakabiliwa na shinikizo la kutoweza kuhudhuria
kwenye mkutano kati ya Nchi za Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya, unaotarajiwa kufanyika
mwezi Aprili 2014.
Wakati huo huo, habari kutoka Zimbabwe zinasema kwamba,
Serikali ya Zimbabwe imewaachilia huru wafungwa elfu mbili waliokuwa wanatumikia vifungo
katika magereza mbali mbali nchini humo. Hii inatokana na hali ngumu ya uchumi pamoja
na makundi ya kutetea haki za binadamu yanayodai kwamba, wafungwa nchini Zimbabwe
wanaishi katika mazingira hatarishi sana na kwamba, wengi wao wanafariki dunia kutokana
na njaa magerezani.