2014-02-18 10:53:40

Mshikamano wa biashara miongoni mwa wanawake wa Eneo la Maziwa Makuu


Jimbo Katoliki la Kyangugu, lililoko nchini Rwanda hivi karibuni lilizindua mfumo wa biashara unaopania kujenga na kudumisha mshikamano wa amani nchini Rwanda, kwa kuwajengea wanawake uwezo katika masuala ya kiuchumi.

Mradi utawashirikisha pia wanawake kutoka eneo la Maziwa Makuu kwani hawa ndio waathirika wa vita na kinzani za kijamii zinapojitokeza katika nchi zao. Burundi na DRC ni kati ya nchi zitakazohusishwa kwenye mradi huu unaotarajiwa kutekelezwa katika kipindi cha miaka miwili.

Baraza la Maaskofu Katoliki Rwanda linasema kwamba, jumla ya wanawake sitini kutoka katika Majimbo kadhaa ya Kanisa Katoliki Eneo la Maziwa Makuu watahusishwa katika biashara ya mshikamano kwa kubadilishana biadhaa kama njia ya ujenzi wa umoja, upendo na mshikamano kati ya watu. Askofu Jean Damascene Bimenyimana wa Jimbo Katoliki Kyangugu, Rwanda anasema, mradi wa Cosopax ni chombo cha kukuzia umoja, urafiki na mshikamano miongoni mwa wanawake wa eneo la Maziwa Makuu.

Hizi ni juhudi zinazochangiwa na Jumuiya ya Kimataifa kwa njia ya mshikamano wa kidiplomasia pamoja na wanasiasa kutoka Eneo la Maziwa Makuu. Tume ya haki na amani, Jimbo Katoliki la Kyangungu ndiyo iliyopewa dhamana ya kufuatilia utekelezaji wa mradi huu miongoni mwa wanawake.

Ni mradi unaojikita katika umoja, upendo, haki na mshikamano wa dhati kati ya wanawake ambao kimsingi ni wajenzi wa amani na uvumilivu. Wanawake wakiwezeshwa kiuchumi na kielimu wanaweza kufanya makubwa zaidi katika Jamii zao.







All the contents on this site are copyrighted ©.