Zingatieni mambo msingi kwa mafao ya watanzania wote wakati wa kujadili muswada wa
Katiba Mpya!
Rais Jakaya Mrisho Kikwete wa Tanzania hivi karibuni alipokuwa anazungumza kwenye
kikao cha Baraza la Vyama vya Siasa nchini Tanzania alisema kwamba,
Bunge la
Katiba ndilo lenye mamlaka ya kutunga Katiba mpya ya nchi ya Tanzania. Hatua zote
zilizopita ni za kutoa mapendekezo jukumu ambalo Tume ya Mabadiliko ya Katiba imelikamilisha
vyema. Ipo Rasimu ya Katiba itakayofikishwa kwenye Bunge Maalum kujadiliwa na kufanyiwa
uamuzi. Ingekuwa Bunge la kawaida au Baraza la Wawakilishi, Rasimu ya Katiba ndiyo
Muswada wa Sheria utakaofikishwa Bungeni na kwenye Baraza.
Wajumbe wa Bunge
hilo watambue kuwa wana dhamana isiyokuwa na mfano wake kwa nchi yetu na Watanzania
wenzao kwa jumla. Wanalo jukumu la kuwapatia Katiba nzuri itakayodumu kwa zaidi ya
miaka 50 ijayo. Katiba itakayoimarisha Muungano badala ya kuudhoofisha. Katiba itakayodumisha
umoja, amani na utulivu nchini badala ya kuvuruga.
Vilevile Katiba itakayoweka
mazingira mazuri ya kisiasa, kijamii na kiuchumi na kuongeza kasi ya maendeleo ya
nchi yetu na ustawi wa watu wake kwa miaka mingi ijayo. Ili haya yafanyike ni vyema
Wajumbe wajue vyema kinachopendekezwa, wapambanue kinachofaa na kisichofaa, na kubwa
zaidi, watangulize maslahi ya taifa mbele kuliko maslahi yao binafsi au ya makundi
yao.