2014-02-17 10:56:02

Kiwango na ubora wa elimu Congo unaporomoka kwa kasi ya ajabu!


Mpango wa elimu kitaifa hauna budi kupewa kipaumbele cha kwanza na Serikali ya Congo Brazzaville pamoja na wadau mbali mbali katika sekta ya elimu. Hii inatokana na ukweli kwamba, elimu ni chanzo cha maarifa na msingi wa maendeleo endelevu kwa taifa lolote lile.

Ikiwa kama Serikali na wadau mbali mbali watashindindwa kuwekeza katika sekta ya elimu, kuha hatari kwamba, Taifa linaweza kujikuta likirudi nyuma katika mchakato wa maendeleo ya watu wake: kiroho na kimwili!

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Baraza la Maaskofu Katoliki Congo Brazzaville katika mkutano wao wa mwaka uliojikita kwa namna ya pekee katika mchakato wa maboresho ya elimu nchini Congo. Kiwango cha elimu kinachotolewa nchini Congo hakikdhi mahitaji ya wananchi wake, hii inatokana na ukosefu wa waalimu wenye viwango na ubora unaohitajika; ukosefu wa miundo mbinu ya kufundishia pamoja na vitabu vya kiada. Idadi kubwa ya wanafunzi wanaofanya mitihani ya kuhitimu kidato cha nne wanashindwa kufaulu vyema kutokana na kasoro mbali mbali zinazojitokeza katika mfumo mzima wa elimu nchini Congo.

Viwango na ubora wa elimu nchini Congo vinaendelea kuporomoka siku hadi siku kiasi kwamba, Maaskofu wanaonesha wasi wasi kwa vijana wanaoelimishwa nchini humo kuweza kumudu pilika pilika za maisha kwa siku za usoni. Kanisa Katoliki litaendelea kuchangia katika maboresho ya sekta ya elimu kwa ajili ya mafao ya wengi nchini Congo na kwamba, Serikali na wadu mbali mbali wanapaswa kuchangia kwa ajili ya mchakato huu wa maboresho ili kuweza kulinusuru taifa kutumbukia katika janga la ujinga kwa siku za usoni.

Baraza la Maaskofu Katoliki Congo linasema, hii ni tafakari ya kina iliyotolewa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, katika Waraka wake wa Kichungaji, Africae Munus, Dhamana ya Afrika. Hapa Kanisa linawachangamotisha wadau kuhakikisha kwamba, wanatoa elimu makini kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa haki msingi kwa watoto Barani Afrika. Bila ya Serikali kuwa na mikakati makini ya elimu si rahisi kuweza kupata maendeleo endelevu yanayogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.







All the contents on this site are copyrighted ©.