Jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa litaendelea kuwepo nchini Burundi hadi
Desemba 2014
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeamua kwamba, Vikosi vya Jeshi la kulinda
amani la Umoja wa Mataifa vitaendelea kuwepo nchini Burundi hadi kufikia Mwezi Desemba
2014 kutokana na hali ya ulinzi na usalama kuanza kutetereka. Jeshi la Umoja wa Mataifa
pamoja na mambo mengine limepewa dhamana ya kuhakikisha kwamba, mchakato wa uchaguzi
mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini Burundi kunako mwaka 2015 unakwenda vyema. Hiki
kitakuwa ni kipimo cha amani na utulivu kwa Burundi.
Baraza la Usalama la Umoja
wa Mataifa limeridhika na hatua mbali mbali ambazo zimechukuliwa na Serikali ya Burundi
katika kukabiliana na vikwazo vilivyojitokeza nchini humo mara baada ya vita ya wenyewe
kwa wenyewe iliyosababisha majanga makubwa kwa watu na mali yao. Mabadiliko ya Katiba
na tetesi za kutaka Rais Pierre Nkurunzinza aliyekuwepo madarakani tangu Mwaka 2005
kupewa tena nafasi ya kuiongoza Burundi kwa kipindi kingine cha awamu ya tatu, jambo
ambalo ni kinyume cha Katiba ya Burundi.
Serikali ya Burundi inapinga wazo
la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuendelea kuwepo nchini Burundi.