2014-02-17 12:01:19

Askofu Gervas Nyaisonga ateuliwa kuwa Askofu Mpya wa Jimbo katoliki Mpanda, Tanzania


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu Gervas Nyaisonga kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Mpanda, Tanzania. Itakumbukwa kwamba, Jimbo Katoliki Mpanda lilikuwa wazi baada ya kufariki dunia kwa Askofu Pascal Kikoti hapo tarehe 28 Agosti 2012.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, tarehe 9 Januari, 2011 alimteua Mheshimiwa Padre Gervas Nyaisonga kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Dodoma, baada ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kumhamisha Askofu Yuda Thadeus Ruwaichi toka Jimbo Katoliki la Dodoma na kwenda Jimbo kuu la Mwanza kama Askofu mkuu.

Askofu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga aliwewa kuwekwa wakfu kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Dodoma, hapo tarehe 19 Marchi, 2011, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo wa Msalaba.

Askofu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, alizaliwa kunako tarehe 3 Novemba, 1966, Wilayani Bunda, Mkoani Mara. Baada ya masomo yake ya msingi na sekondari, huko Mbeya na Sumbawanga, kunako Mwaka 1989 alijiunga na Seminari kuu ya Kibosho, Moshi, kwa ajili ya masomo ya Falsafa na baadaye akaendelea na masomo ya Kitaalimungu huko Segerea, Jimbo kuu la Dar es Salaam na hatimaye, kuwekewa mikono kama Shemasi, kunako mwaka 1995 baada ya kumaliza mwaka wa kichungaji, alioufanya katika Parokia ya Itaka, Jimbo Katoliki la Mbeya

Na tarehe 11 Julai, 1996 akapewa daraja takatifu ya Upadre, Jimbo Katoliki la Mbeya na Hayati Askofu Yakobo Dominic Sangu. Historia inaonesha kwamba, huyu ndiye aliyekuwa Padre wa mwisho kuwekewa mikono na Askofu Sangu. Baada ya Upadrisho alifanya utume katika sehemu mbalimbali za Jimbo Katoliki Mbeya, kama Paroko msaidizi, huko Itumba na Mwalimu wa Seminari Ndogo ya Mbalizi. Kuanzia mwaka 1998 hadi mwaka 2001 alijiendeleza kwa masomo ya juu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania, ambako alijipatia shahada ya kwanza. Baada ya masomo yake, alirudi kuendelea na kazi yake kama Mkuu wa shule ya Sekondari ya Pandahill, kuanzia mwaka 2001 hadi mwaka 2006.

Kuanzia mwaka 2006 hadi mwaka 2009 alijiendeleza kwa masomo ya juu zaidi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alikojipatia Shahada ya uzamili katika masomo ya Sayansi Jamii. Kuanzia mwaka 2009 hadi kuteuliwa kwake, alikuwa ni Mhadhiri Msaidizi katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino cha Tanzania, SAUT, kilichoko Jijini Mwanza. Akiwa SAUT, kunako Mwezi Agosti, 2010, alitumwa nchini Ujerumani kwa masomo ya juu zaidi, kama sehemu ya maandalizi ya kuwa ni Jaalimu wa Elimu hasa katika somo la Jiografia. Kabla ya kuhitimu masomo yake huko Ujerumani, akapokea simu kutoka kwa Balozi wa Vatican nchini Tanzania, ikimtaarifu uteuzi wake kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Dodoma.

Askofu mteule Gervas Nyaisonga anasimulia kwamba, wito wake kama Mkatoliki na baadaye kama Padre na sasa kama Askofu ni mchango mkubwa alioupokea kutoka kwa wazazi wake na kwa namna ya pekee Mama yake Mzazi aliyekuwa n anafasi ya pekee katika malezi. Huyu alikuwa kwa hakika ni Mwalimu na katekista wa kwanza katika majiundo yake ya maisha ya kiroho. Hii inatokana na ukweli kwamba, Baba yake Mzazi hakuweza kuwa nyumbani wakati wote kutokana na dhamana na utumishi wake kwa umma.
Tangu akiwa mtoto mdogo alitamani na akapenda kutumia Altareni pamoja na kusoma masomo Kanisani wakati wa Liturjia ya Neno la Mungu. Alipofikia umri wa kujiunga na Seminari ndogo, yeye alikuwa ni kati ya vijana kumi waliochaguliwa kutoka Parokiani mwake, lakini kati yao wawili tu, ndio waliobahatika kufikia Daraja Takatifu la Upadre, yaani Yeye Askofu na Padre Januari Mwilwa wa Jimbo Katoliki Mbeya.
Akiwa Seminari ndogo wito na ari ya kujitoa kwa ajili ya kumtumikia Mungu na jirani viliendelea kukua na kukomaa taratibu, akijikita zaidi katika maisha ya: Sala, Masomo, Kazi na Michezo, kama sehemu ya vipaumbele wakati wa malezi Seminarini. Ni mahali alipokuza vipaji vyake kwa ajili yake mwenyewe na Kanisa kwa ujumla. Akaendelea kukua katika kimo na busara sanjari na kukomaa kwa wito wake, akitamani daima kuwa Padre. Alipohitimu masomo ya kidato cha sita, alishawishiwa na walimu wake kwenda Jeshi la Kujenga Taifa kwa mujibu wa sheria, ili baadaye, aweze kujiunga na Chuo Kikuu kwa masomo ya juu zaidi.
Mkurugenzi wa miito hakucheza mbali na vijana wake, akamshauri kujiunga na Seminari kuu kwa ajili ya kuendelea na masomo ya kipadre, ushauri huu ukajikita katika moyo wake, akapiga moyo konde na kwenda Seminarini. Kwa sasa anamwimbia Mungu utenzi wa shukrani kwa matendo makuu aliyomtendea katika hija ya maisha yake kama Padre, Askofu wa Jimbo Katoliki Dodoma na sasa aka Askofu wa Jimbo Katoliki Mpanda.

Imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.