2014-02-15 14:03:24

Wazee, hazina ya familia na Jamii....


Tunaendelea kujielimisha na masuala mbalimbali yanayohusiana na maisha mchanganyiko, tukiwa ndani ya familia ambamo kwa kawaida tuna baba , mama, watoto na wazee na wagonjwa. Wanasayansi wanasema kuzeeka ni suala la maendeleo kimaisha. Wazee ni chemchemi ya maisha ya familia , jumuiya na hata katika mipango ya kijamii na kiuchumi.

Katika vipindi vya nyuma tumewazungumzia , Baba na mama kama wakuu wa familia kwamba, wana wajibu muhimu wa kujua kila hali na maendeleo ya kila mwana familia, kimaisha na kiroho pia. Na ni wajibu wa watoto kuheshimu mila na desturi za wazazi wao.

Leo, tunawazungumzia wazee , tunaoishi nao katika familia hata nje ya familia, wao kama watangulizi wetu katika maisha. Tunawaheshimu tena kwa ufahamu kwamba, kuishi kwao miaka mingi wamepata uzoefu wa kutosha kimaisha na wameona mengi pia na hivyo wanakuwa ni hazina kubwa kwa vizazi vipya.

Wanasayansi wanasema kuzeeka ni suala la maendeleo kimaisha. Wazee ni chemchemi ya furaha na mafanikio ya maisha katika familia , jumuiya na hata katika mipango ya kijamii na kiuchumi.

Kwa kujali umuhimu wa kundi hili la watu wazee ambao ni vijana wa juzi , Umoja wa Mataifa uliitangaza tarehe Moja Oktoba kuwa Siku ya Kimataifa ya Wazee.

Baraza la Kipapa kwa ajili ya Walei katika waraka wake wa kichungajiwa 1 Oktoba 1998, juu ya heshima ya watu wazee na utume wao katika kanisa, unaeleza kwamba, Maendeleo ya kisayansi, hasa maendeleo katika uwanja wa tiba na dawa, umechangia kwa kiasi kubwa katika miongo ya hivi karibuni, kuongeza muda wa wastani wa maisha ya binadamu. Uwepo wa kizazi cha tatu, imekuwa sehemu kubwa ya idadi ya watu duniani : watu wastaafu katika kazi ya ajira ya kazi, lakini, wanabaki kuwa rasilimali kubwa ndani ya familia , wakiwa na uwezo wa kutoa mchango kwa manufaa ya familia na umma.

Kwa mujibu wa habari za watu , watu wanaostahili kuwekwa katika kundi la kuitwa wazee ambao majuzi walikuwa ni Vijana, ni watu walio katika umri wa miaka kati ya 65 hadi 75. Baada ya miaka hiyo mtu anapata heshima zaidi ya kuitwa mkongwe.

Kanisa pamoja na kufurahia mwendelezo wa wastani wa kuishi watu , pia linahofia kupungua kwa kiwango kikubwa cha watu wanaozaliwa yaani watoto. Katika ukweli wake, ikilinganishwa na miaka ya nyuma kwa wakati huu inakwenda kinyume kwamba idadi ya wazee inakuwa kubwa kuliko idadi ya vijana na watoto ,kama inavyo onekana katika grafu ya idadi ya watu dunianiya Umoja wa Mataifa kwa mwaka 2002. Idadi ya wazee inazidi kuongezeka , wakati vijana wanapungua. Mabadiliko haya yaliyoanza katika nchi za Kaskazini mwa Dunia kwa sasa yana enea kwa kasi sana katika ulimwengu wa Kusini.

Nalo Shirika la Afya la Dunia (WHO) katika taarifa yake ya March 28, 2012 ilidhihirisha kwamba, Idadi ya watu duniani iko katika kasi ya kuzeeka, kwamba kati ya mwaka 2000 na 2050 , idadi ya watu duniani walio na umri wa zaidi ya miaka 60 itakuwa mara mbili kutoka asilimia 11% hadi 22%. Idadi kamili ya watu wenye umri wa miaka 60 na zaidi linatarajiwa kuongezeka kutoka millioni 605 millioni hadi billioni 2 katika kipindi hicho. Na kwamba nchi za kipato cha kati zitaona mabadiliko haya kwa kasi zaidi.

Ripoti ya WHO inaendelea kusema Dunia katika miongo michache ijayo itakuwa na watu zaidi wenye umri wa miaka 80 na 90 zaidi kuliko ilivyokuwa kabla. Kihistoria dunia haijawahi kushuhudia uwepo wa watu wenye wengi umri wa kati na watu wazima, idadi iliyo zaidi ya watoto. Huu ni uzoefu mpya, wazazi kuendelea kuwa hai, kama ilivyo leo, watoto kuwaona wazazi wao, mababu na mabibi zao na hata Mabibi na Baba wakubwa.Kwa wastani, wanawake huishi miaka sita hadi nane zaidi ya wanaume.

Na kwa jinsi gani , umri mkubwa unavyoweza kuwa mzuri na wa manufaa, inategemea sababu nyingi, ikiwemo uwezo wa kazi wa mtu binafsi katika mfumo wake wa kibiolojia , ikiwemo pia tabia na maambukizi katika maisha, bila ya kusahau kile mtu anacho kula , anachofanya na uwezo wa kujikinga na hatari za afya kama zile zinazo sababishwa na sigara, matumizi ya pombe, au sumu nyingine.

Taarifa pia inasema, kimataifa, watu wengi zaidi hufariki mapema kutokana na huduma mbovu. Karibia 4-6% ya wazee katika nchi zilizoendelea wamesha kumbana na matatizo ya kutendewa vibaya nyumbani .Hata katika taasisi wazee wengi hupambana na kukemewa, kutukanwa , na hasa wenye wazee wagonjwa wasio jiweza kimwili, hunyima hadhi ya utu wao (kwa mfano kwa kuwaacha katika nguo chafu, kunyimwa chakula, kutosikilizwa haja na moni yao, kunyimwa haki ya kuchagua wnachopenda n,k ) . Tafiti juu ya mambo ya wazee zinaonyesha kwamba, vitendo viovu dhidi ya wazee husababisha majeraha makubwa ya kimwili na Kisaikolojia kwa muda mrefu .

Mama Kanisa kwa sasa anajali kwamba, Idadi hii kubwa ya watu wazima kwa sasa, baada ya kupita miongo miwili mitatu, watakuwa na uwezo mdogo wa kujihudumia kama tulivyoelezwa kwamba , katika nchi zinazoendelea, inatabiriwa idadi ya wazee itaongezeka kwa mara nne zaidi ifikapo mwaka 2050. Kutakuwa na wazee wengi na wakongwe, waliopoteza uwezo wao wa kuishi kwa kujitegemea wenyewe kwa sababu mbalimbali kama uhamiaji, udhaifu kutokana na maradhi au matatizo mengine ya kimwili au kiakili . Na hivyo wengi wao watakuwa wakihitaji huduma ya muda mrefu kutoka kwa vijana, ambao nao idadi yao haitakidhi mahitaji ya wingi wa wazee wanaohitaji kuhudumiwa. Upungufu huu wa vijana, unatokana na wazee hao kukataa kuzaa kwa makusudi ya kukwepa usumbufu, ubinafsi na ubahiri.. Hata kama kutakuwa na nyumba za kuwaweka wazee pamoja, bado makazi hayo yatahita kuhudumiwa na jamii ,kusaidiwa kimaisha.

Taarifa inazidi kuogopesha kwamba, kuna hatari wazee wengi kupatwa na maradhi ya akili, hasa kutokana na upweke, ikikadiriwa kuwa asilimia 25-30 % ya watu wenye umri wa miaka 85 au zaidi, watapatwa na maradhi ya akili hasa ugonjwa a kusahau na utambuzi . Mpaka sasa wazee wenye shida hii ya akili hasa katika nchi za kipato cha kati na chini , wengi wao hawapati huduma endelevu katika taasisi za kiserikali . Mara nyingi uzito wa maatizo ya wazee, hubebwa na familia zao, huwafadhili na kuwahudumia nyumbani. Ikiwa ndivyo, Je itakuwaje kwa wazima wa sasa wanaokata kuzaa watoto kwa makusudi, wakati watakapofikia umri huo mkubwa ? Ina maafa watabaki peke yao majumbani bila huduma, na pia hakuna mwendelezo wa kizazi. Hivyo unakuwa ni mwisho wa familia yake katika uso wa dunia.

Na katika hali ya dharura, wazee huathirika zaidi , mfano kunapotokea majanga asilia au vita, wazee na wakongwe hawawezi kukimbia haraka au kusafiri umbali mrefu na hivyo huachwa nyuma wakiteseka, licha ya kuwa rasilimali muhimu kwa jamii zao na pia kama chemchemi ya mawazo katika mchakato wa misaada ya kibinadamu, katika ushiriki wao kama viongozi wa jamii

Kwa kujali upungufu wa kizazi kipya, Kanisa linasema, hii ni changamoto kwa dunia, inayohitaji mapinduzi ya haraka, vinginevyo ni kiama cha dunia. Dunia inapaswa kufanya mapinduzi ya katika suala hili idadi ya vijana kuzidi kushuka, vinginevyo itasababisha matatizo ya kijamii , kiuchumi, kiutamaduni , kisaikolojia na kiroho.

Katikati ya mwaka 1982, Dunia ilifanya mkutano wa Kimataifa juu ya Wazee uhuko Vienna , Austria, mkutano uliobaki kuwa rejea katika kumbukumbu za Kimataifa, juu ya wazee.

Katika makalamengine yatayofuatia tutatazama matokeo ya majadiliano mbalimbali yaliyofanywa na Umoja wa Mataifa, ambayo yametoa Kanuni mbalimbali juu ya kundi la watu wazee.

Makala Dunia Mama huandaliwa nami Tjmhella







All the contents on this site are copyrighted ©.