Tokeni kifua mbele kutangaza Habari Njema ya Wokovu na wala msiogope wala kuona soni!
Baba Mtakatifu Francisko ameitaka Jumuiya ya Kikatoliki ya Shalom kupiga moyo konde
na kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu ili kutangaza Habari Njema ya Wokovu pasi na
woga wala makunyanzi! Baba Mtakatifu ameyasema hayo alipokutana na Muasisi wa Jumuiya
ya Kikatoliki ya Shalom Moyses de Azevedo Filho, kwenye Makazi yake yaliyoko kwenye
Hosteli ya Mtakatifu Martha, yaliyoko mjini Vatican, siku ya Ijumaa tarehe 14 Februari
2014.
Baba Mtakatifu Francisko anaifahamu Jumuiya hii na kwa mara ya kwanza
walikutana kunako Mwaka 2007 wakati wa Maadhimisho ya Mkutano wa Aparecida, nchini
Brazil. Kanisa likaitambua Jumuiya hii na kuipatia hadhi yake ndani ya Kanisa, kama
kumbukumbu endelevu ya Hija ya kichungaji ya Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili aliyoifanya
nchini Brazil kunako Mwaka 1980. Leo hii Jumuiya ya Kikatoliki ya Shalom imeenea katika
nchi ishirini na mbili na ina jumla ya wanachama 40, 000.
Akizungumza na Radio
Vatican kwa njia ya simu Bwana Moyses de Azevedo anasema, mazungumzo yake na Baba
Mtakatifu Francisko ilikuwa ni fursa ya kurudia tena majitoleo na sadaka yao kwa ajili
ya kutangaza Injili ya Furaha hadi miisho ya dunia. Jumuiya hii imekwisha anza kuona
matunda ya utume wake kwa Padre Joao Chagas kuteuliwa kuwa ni Mratibu wa Siku za Vijana
Duniani, kwenye Baraza la Kipapa la Walei.
Hii ni neema ambayo Jumuiya ya
Kikatoliki ya Shalom imepata kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya huduma na utume
miongoni mwa vijana, ni uthibitisho wa karama ya Jumuiya hii ambayo inatoa kipaumbele
cha kwanza kwa ustawi na maendeleo ya Kanisa.