2014-02-15 15:06:04

Raslimali ya nchi itumike kwa ajili ya mafao ya wengi!


Kardinali John Onaiyekan wa Jimbo kuu la Abuja, Nigeria, hivi karibuni wakati wa Maadhimisho ya Ibada ya Misa takatifu katika kumbu kumbu ya Jubilee ya Miaka 70 tangu kuzinduliwa kwa Kanisa la Bikira Maria Malkia wa Nigeria, Jimbo kuu la Abuja amewataka viongozi wa Serikali na kutoka katika sekta ya watu binafsi kutumia vyema rasilimali ya nchi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wote wa Nigeria.

Kardinali Onaiyekan anasema kwamba, Mwenyezi Mungu ameikirimia Nigeria utajiri mkubwa wa maliasili ambayo kimsingi inapaswa kutumiwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wote wa Nigeria bila upendeleo, kama kielelezo cha utekelezaji wa misingi ya haki, amani na maendeleo endelevu. Huu unaweza kuwa ni mchango mkubwa katika kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza nchini Nigeria: ukosefu wa amani na utulivu unaoweza kuchangiwa kutokana na umaskini; rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma pamoja na kumong'onyoka kwa tunu msingi za maadili na utu wema.

Matumizi sahihi ya rasilimali ya nchi unaweza kuwa kwelini ufumbuzi wa changamoto zote hizi na chachu ya maendeleo kwa wananchi wengi wa Nigeria ambao kwa sasa wanakwamishwa kutokana na vitendo vya kigaidi vinavyonyanyasa na kuwadhulumu watu wasiokuwa na hatia. Wananchi wa Nigeria wanapaswa kuanza mchakato wa kujikita katika ujenzi wa nchi yao kwa hali na mali badala ya kushiriki kuibomoa.

Kanisa kwa upande wake, litaendelea kusimamia misingi ya maendeleo endelevu kiroho na kimwili; kanuni za maadili na utu wema pamoja na kuchangia juhudi za Uinjilishaji wa kina katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu. Kardinali John Onayeikan anasema, anapenda kujielekeza zaidi katika mambo yanayomfaidisha mwanadamu na kumpendeza Mwenyezi Mungu.







All the contents on this site are copyrighted ©.