Rais wa Cyprus akutana na Papa Francisko mjini Vatican
Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi, tarehe 15 Februari 2014 amekutana na kuzungumza
na Rais Nicos Anastasiades ambaye baadaye alikutana na Kardinali mteule Pietro Parolin,
Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambata na Askofu mkuu Dominique Mamberti, Katibu
mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.
Viongozi
hawa wawili wamejadili pamoja na mambo mengine kuhusu uhusiano kati ya Cyprus na Vatican;
mchango mkubwa unaotolewa na Kanisa Katoliki nchini humo pamoja na umuhimu wa kuendelea
kusimama kidete kulinda na kutetea uhuru wa kidini. Kwa pamoja wameonesha matumaini
makubwa baada ya kuanza tena majadiliano ya kisiasa yanayopania kupata ufumbuzi wa
kudumu kutokana na hali ngumu inayoendelea nchini Cyprus kwa sasa.
Baba Mtakatifu
na mgeni wake wameangalia pia kinzani, migogoro na vita huko Mashariki ya Kati ambayo
imesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Ni matumaini ya viongozi hawa kwamba,
Jumuiya za Kikristo huko Mashariki ya kati zitachangia katika ustawi na maendeleo
ya Ukanda huu.