Shutuma zinazotolewa na baadhi ya wanaharakati dhidi ya Kanisa katoliki kuhusiana
na tunu msingi za kiutu na kimaadili katika masuala kama vile utoaji mimba, vizuia
mimba, matumizi ya viini tete katika majaribio ya kisayansi ni kutokuwa na ufahamu
wa kutosha kuhusu Mafundisho Jamii ya Kanisa.
Kimsingi, Kanisa linajipambanua
katika Mafundisho yake kwa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu
aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; haki na amani pamoja na mafao ya wengi. Kanisa
linapenda kusimamia haki msingi za binadamu. Ni changamoto iliyotolewa hivi karibuni
na Askofu mkuu Ignatius Kaigama wa Jimbo kuu la Jos, Nigeria wakati wa semina maalum
kwa wafanyakazi katika sekta ya afya nchini Nigeria. Semina hii ilikuwa inaongozwa
na kauli mbiu "Huduma ya afya mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa"
Mafundisho
Tanzu ya Kanisa yanapata chimbuko lake katika Biblia na Mapokeo ya Kanisa na hayawezi
kubadilishwa kwa kushinikizwa na Serikali, wanaharakati au watu ambao wameshindwa
kuheshimu na kuthamini sheria asilia, maadili na utu wema. Kuna baadhi ya wanahakati
ndani ya Jamii wanataka kujichukulia sheria mikononi mwao wa kuwa ni vipimo na vigezo
vya maadili na misimamo ya kijamii hata pale wanapokuwa wamepotoka na kukengeuka,
jambo ambalo kamwe haliwezi kukubalika!
Kanisa haliwezi kukubali kushinikizwa
kufungisha ndoa za watu wa jinsia moja kwa mfano kwani hiki ni kinyume kabisa cha
Maandiko Matakatifu, maadili na utu wema. Ni jambo linalokwenda kinyume na mpango
wa Mungu katika maisha ya mwanadamu anayeshirikishwa katika mchakato wa kuzaa na kulea
watoto. Kanisa haliwezi kupindisha Mafundisho yake ili kupata msaada wa fedha zenye
masharti kama inavyojionesha kwa baadhi ya nchi na wahisani wanaotaka kuzilazimisha
nchi za Kiafrika kupitisha sheria zinazokumbatia utamaduni wa kifo kwa kisingizio
cha uhuru na demokrasia na kusahau kwamba, hata uhuru una mipaka na ukomo wake!
Askofu
mkuu Kaigama ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria amewataka Wananchi
wa Nigeria na Afrika katika ujumla wao, kuwa makini na athari za utandawazi zinazoweza
kuwachanganya na kuwavuruga kiasi cha kushindwa kutambua kama kweli ni Waafrika au
wamekwishagenishwa kwa tamaduni za kigeni ambazo baadhi yake zimepotoka na kukengeuka!
Waamini wawe waaminifu na wadumifu katika Mapokeo ya dini zao, mila na desturi njema
za Kiafrika. Wabnanchi hawapaswi kuiga kila jambo analotenda mtu kutoka Ulaya.
Wafanyakazi
katika sekta ya afya wanapaswa kulinda na kutetea: maisha, utu na heshima ya binadamu
na kamwe wasikumbatie utamaduni wa kifo! Waongozwe na kanuni bora za maadili na sheria
za kazi pamoja na kujitabisha kujifunza kanuni msingi za Mafundisho Jamii ya Kanisa.
Madaktari na wauguzi waendelee kutoa huduma hali wakibaki kuwa ni Wakatoliki
waaminifu, waadilifu na wachapa kazi, mfano wa kuigwa na wafanyakazi wengine katika
huduma za kijamii, kwa njia hii watakuwa wanayatakatifuza malimwengu kwa njia ya maisha
na huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.