2014-02-15 15:48:57

Hapa leo ni kuzunguzungu tupu!


Hotuba ya mlimani, ni moja ya fasuli za Injili inayotia kizunguzungu. Ama kweli ni Habari njema itokayo kwa Mungu na siyo kwa binadamu. Kwa upande mmoja, maneno hayo yananifanya nijisikie kushindwa kabisa kuyatekeleza. Lakini kwa upande mwingine najidanganya na kusema: Injili hii haina ugumu wowote wa kuifuata.

Kwa namna fulani ni ukweli, kwani Yesu mwenyewe alishasema: “Njoni kwangu, ninyi nyote mliochoka na kuonewa nami nitawapumzisha.” (Mt. 11:28) Maneno hayo ya Yesu hayaaliki watu pekee na maarufu katika maisha, bali yanawaalika watu wa kawaida wanaume kwa wanawake mimi nikiwa mmojawao.
Lakini maneno ya leo ya Yesu yanatia kizungunzugu:

Hebu tukielezee kwanza hicho kizunguzungu kwa kuanza na maneno ya Yesu pale anapotamka neno torati. Anasema: “Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati la hasha, bali kutimiliza.” Torati ina maana nyingi, maana mojawapo inayozoelekea ni sheria. Lakini maana halisi ni mwongozi, au dira. Kiasili neno torati linamaanisha mshale ule unaorushwa kuonesha upande wa kuelekea. Kwa wawindaji na mbwa, maana hii itaeleweka vizuri sana kwao ukilinganisha na mshale au jiwe analorusha mwindaji kuelekea aliko mnyama anayewindwa ili mbwa aweze kuelekea huko na kumfukuza mnyama huyo. Au wakati mwingine mwindaji anapiga mluzi na kuonesha kwa kidole upande alikoelekea mnyama.


Endapo mbwa hajafundishwa sawasawa kuwinda, mwindaji anapoonesha kidole kuelekea aliko mnyama, mbwa ndiyo kwanza anakalia mkia na kukiangalia kidole cha bwana wake. Mbaya zaidi mbwa mwingine anaanza kurukia panzi walio pale jirani. Hapo mbwa huyo amepata kizunguzungu, na haelewi kinachotakiwa. Yesu amefika kuikamilisha torati, siyo kuitangua, maana yake, tayari torati imeshatuonesha upande mzuri wa kuelekea, Yeye amekuja kuendeleza pale ulipotua mshale na kusaidia kufikia ilipo hazina au uhondo, yaani utakatifu.

Hapo ndipo Injili au ujumbe wa Yesu inapotia kizunguzungu. Hebu tuone jinsi Yesu anavyotupelekesha katika Injili ya leo ili kuelekea mbele zaidi ya kule unakotuonesha mshale - torati:

“Mmesikia imesemwa…bali mimi ninawaambieni.” Yesu hatangazi maadili mapya na ya pekee, na wala hadokezi sheria mpya yenye kutubana zaidi. Yeye hatungi katiba mpya, kwani anajua katiba iliyoko ni mwongozo tosha, ni torati, ni mshale, unaotuelekeza upande unaofaa. Kwa hiyo hayo ni maneno ya Injili yaliyo ya msingi, ni maneno ya kiutu, kwani yanaonesha msingi wa maisha mazuri na yanatufundisha kuwaza pakubwa, kwa ajili yetu na kwa ajili ya historia ya maisha yetu.


Lakini maisha hayo mazuri na bora yanapatikana kwa kufuata maelekezo mawili anayoyadokeza Yesu: Maelekezo hayo yanagusa undani wa moyo wa mtu na mengine yanaelekezwa kwenye nafsi au utu wa mtu.
Dokezo la kwanza na la msingi la Yesu ni kule kurudi kwenye moyo na kujitafakari: Nani ya moyo ndiyo kunakoundwa kile kitakachomtoka mtu kama vile neno, tendo, ishara iwayo yoteyote ile: kwa hiyo yabidi kwanza kuuweka sawa huo moyo na kuuponya, ili kuweza kuponya maisha. Hivi Yesu anatuingiza kwenye kizunguzungu cha pili anaposema:

“Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiue. Bali mimi nawaambieni, kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu.” Yaani yeyote anayefuga ndani ya moyo wake hasira na chuki, “tayari huyo ni mwuaji”. Maana yake, Yesu anaenda kwanza kwenye kiini, kinachosababisha au kinachounda maisha. Kile ambacho Yohane anakithibitisha: “Asiyempenda ndugu yake huyo ni mwuaji.” (IYoh.3:15). Kutompenda mwingine, huko tayari ni kutoa maisha; kwa hiyo yeyote asiyependa, anamwua mwingine, na anajiua yeye mwenyewe. Yaani kutopenda kwako e tayari ni kifo cha polepole hicho. Hicho ni kizunguzungu cha kutosha kumwangusha mtu.

Kizunguzungu cha tatu, Yesu anasema: “Mimi nawaambieni msiape kabisa; Bali maneno yenu yawe Ndiyo, ndiyo; Siyo, siyo; kwa kuwa yazidiyo hayo yatoka kwa yule mwovu.” Huko kukataza kuapia, Yesu anataka kukataza kubomoa uwongo. Sema kweli daima na hutahitaji kuapa. Yesu anapelekesha kwenye ukamilifu, moyoni, matokeo yote yaliyofikiriwa katika sheria ya zamani.

Kisha Yesu anatuletea kizunguzungu cha nne kinachoelekezwa kwa nafsi au utu wa mtu pale anaposema: “Mmesikia kwamba imenenwa usizini; mimi nawaambia, kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake.” Yesu hasemi kikawaida tu; kwamba endapo mwanamme unamtamani mwanamke, au endapo wmwanamke unamtamani mwanamume. La hasha, kwa sababu inaeleweka kabisa kwamba kutamani ni kwa lazima ingawaje ni utumwa na unyonge wa namna lakini ni muhimu kutamani.

Yesu kumbe anasema: “Unamwangalia kwa kutamani.” Kama unaangalia tu kwa ajili ya hamu zako, ka unauangalia mwili wako kwa ajili ya kujifurahisha tu; hapo ndugu yangu unatenda dhambi dhidi ya nafsi au utu. Hapo wewe ni mzinzi, kwa maana halisi ya neno: Unachafua, unadanganya, unaifukarisha nafsi hiyo. Kwa sababu unamdhalilisha toka hali yake ya utu na kumshusha hadi kwenye kiwango cha kitu kwa ajili ya matumizi yako binafsi. Kwenye kiwango cha mwili wa kuutumia kisha kuutupilia mbali, bila kutambua kwamba binadamu au mtu huyo ni kitu kikubwa sana, bahari kubwa na pana, ni mbingu, ni malaika, ni mjumbe, ni kina, ni kizunguzungu hicho. Hapo unatenda dhambi zaidi ya kuvunja sheria, bali dhidi ya ukina, undani, na uheshima, wa utu wa binadamu.

Hapo hujaenda zaidi ya inakotuelekeza sheria, torati na katiba, yaani ni ufunuo na mwongozo wa kumfanya mtu akue kiutu wake na kutufunulia tuone kile kinachodhalilisha utu na ukuu wa mtu; yaani, ni ufunuo wa kile kinachompa mtu furaha. Na kitu hicho kipo ndani yetu. Hapa kizunguzungu kitaeleweka zaidi kwetu endapo tutakumbuka kizunguzungu kilichomtokea kipofu yule wa Bethsaida aliyeponywa na Yesu na halafu akamwuliza: “Unaona nini?” kipofu akamjibu: “Naona watu kama miti inatembea” Yaani anaona watu kama vitu tu.

Hicho ni kizunguzungu kilichogeuka kuwa homa. Hapo Yesu akaona aingilie tena upya kazi ya uponyi, akaweka mikono machoni pa kipofu, naye akaweza sasa kusema vizuri kwamba: “Sasa ndiyo naona watu, sura ya Mungu.” (Mk.8:22-26). Kwa sababu huyu ni binadamu: ni umbo la Mungu, anayetembea. Endapo wewe unamwangalia kwa kumtamani kwa kutaka kummiliki hapo upo unausharatisha ukuu wa nafsi ile, iliyo mfano wa Mungu.

Hii ni hatua pekee ambayo Yesu anaipendekeza hapa, ni hatua ya msingi sana: kwenda mbele zaidi ya ulipotua mshale, katiba, sheria (torah) hadi kumwelekea binadamu, kutoka nje ya binadamu, hadi undani na utu wake halisi, toka kwenye dini ya kutekeleza mambo kwa njenje tu bali hadi kwenye dini ya kuwepo. Kutoka kwenye hali ya kuishabikiashabikia tu dini, bali hadi kwenye kuwa mwanadini.

Kosa kubwa sana tulifanyalo binadamu, tena kosa baya sana, ni kule kujionesha kwa nje, kile kinachodunda ndani ya moyo. Kwa hiyo, haitoshi tu kutawala matendo yanayoonekana kwa nje, bali muhimu zaidi ni kuifanyia kazi sana nafsi yako mwenyewe, kukifanyia kazi kile kinachodunda ndani ya moyo wako. Uingie ndani ya moyo wako mwenyewe. Katika kipengee hiki, Injili inakuwa kitu rahisi, yaani kujenga utu, hata kama injili hiyo inatamka maneno yanayoletesha kizunguzungu.

Huwi wa kwanza kwani hata Mama Maria alipata kizunguzungu siku ile alipotokewa na malaika Gabrieli, lakini akasema: “Mapenzi yako yatimizwe” (Luka 1:38), yaani unibadilishe moyo wangu, uniunde kwa mikono yako, mimi ni udongo wako wa mfinyanzi. Na akamzaa Mungu. Tunaweza kufanya hata sisi. Kuzaa upendo katika ulimwengu huu.

Pale tutakapokuwa katika hatari,
Hatari inayotia kizunguzungu,
Utuvutie sisi kwako;
tusipate kizunguzungu,
utufanye watakatifu halisi,
wavumilivu halisi,
na utufanye sisi,
tuwe jiwe la upendo,
ambalo linadumu hata baada ya kifo.

Tafakari hii imetayarishwa na
Padre Alcuin Nyirenda.








All the contents on this site are copyrighted ©.