2014-02-14 15:17:35

Waamini wawezeshwe kukutana na Kristo kwa njia ya Neno na Sakramenti za Kanisa


Khalifa wa Mtakatifu Petro ataendelea kuonesha mshikamano wa dhati na waamini katika shida na mhangaiko yao; matumaini na wasi wasi wao; wakati wa raha na shida. Hija za kitume zinazofanywa na Maaskofu Katoliki mjini Vatican zinamwezesha Papa kufahamu hali ya Makanisa mahalia, tayari kusonga mbele kwa imani na matumaini katika dhamana ya Uinjilishaji Mpya.

Imani ya Waamini wa Kanisa Katoliki nchini Cheki inapata chimbuko lake wakati wa Uinjilishaji uliofanywa na Watakatifu Cyril na Metodi, sasa ni jukumu la kila mwamini kumwilisha historia hii katika maisha yake. Hayo yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati alipokutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Cheki linalofanya hija yake ya kitume mjini Vatican.

Baba Mtakatifu amekazia kwa namna ya pekee umuhimu wa kila mwamini kukutana na Kristo kwa njia ya Sakramenti za Kanisa pamoja na ushiriki mkamilifu katika Liturujia ya Kanisa, mambo yanayohitaji majiundo makini. Ameyapongeza Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume yanayoendelea kutekeleza dhamana na wajibu wake katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu: kiroho na kimwili.

Waamini wanapaswa kujenga na kuimarisha mshikamano na Makleri ili kwa pamoja waweze kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kuwatangazia watu Injili ya Furaha. Baada ya madhulumu ya utawala wa kikomunisti, kuna haja kwa Kanisa kujikita katika majadiliano ya kina na wadau mbali mbali; kuendelea kumwilisha tunu msingi za maisha ya Kiinjili na Kiutu sanjari na kuwafunda wananchi ili waweze kuwa ni vyombo vya: haki, amani na upatanisho; daima wakisimama kidete kutafuta mafao ya wengi na huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Baba Mtakatifu anawahimiza Maaskofu kuhakikisha kwamba, wanatekeleza utume wao wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa upendo na ukarimu kwa kuwajali na kuwasaidia Makleri wao ambao ni wasaidizi wao kwa kwanza katika huduma kwa watu wa Mungu.

Kanisa liendelee kuwekeza katika mikakati ya shughuli za kichungaji miongoni mwa vijana ili kukuza miito mitakatifu. Familia ipewe kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Kanisa; waamini wawe tayari kushuhudia tunu msingi za maisha ya Kikristo hata katika maisha ya hadhara na kwenye vyombo mbali mbali vya mawasiliano ya kijamii.

Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu kujenga na kuimarisha mshikamano wa dhati kati yao ili kukabiliana na changamoto za maisha kwa pamoja. Rasilimali mbali mbali zinazomilikiwa na Kanisa ziwe ni kwa ajili ya utume na maisha ya Kanisa. Mali ya Kanisa itumike kwa kuzingatia misingi ya ukweli na uwazi; weledi, nidhamu na taaluma.







All the contents on this site are copyrighted ©.