2014-02-14 15:27:16

"Tuungeni mkono kupambana na ujangiri Barani Afrika"


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameitaka Jumuia ya Kimataifa kusaidia kukomesha na kufunga masoko ya pembe za tembo na faru kama moja ya njia za kukomesha mauaji na biashara haramu ya wanyapori hawa.

Akizungumza, Alhamisi, Februari 13, 2014 kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Kukabiliana na Ujangili na Biashara Haramu ya Pembe za Tembo kwenye Jumba la Lancaster mjini London, Rais Kikwete amesema kuwa bila kufunga masoko hayo kazi ya kudhibiti ujangili na mauaji ya wanyamapori hao itakuwa ngumu.

Rais Kikwete alikuwa mmoja wa viongozi wa Afrika ambao walizungumza kwenye ufunguzi wa Mkutano huo uliohudhuriwa na wakuu wa Serikali na nchi pamoja na wawakilishi wa nchi 60 duniani. Mkutano huo umeandaliwa na Serikali ya Uingereza kwa ombi la Mtoto wa Malkia wa Uingereza, Prince Charles.

Mbali na Rais Kikwete, viongozi wengine wa Afrika walioshiriki Mkutano huo na kuzungumza ni pamoja na Rais wa Botswana Mheshimiwa Jenerali Khama Iam Khama, Rais wa Gabon Mheshimiwa Ali Omar Bongo na Rais wa Chad Mheshimiwa Idrissa Deby. Ethiopia iliwakilishwa na Waziri.

Rais Kikwete amewaambia mamia ya wajumbe wa Mkutano huo: “Mwisho, nataka kuiomba Jumuia ya Kimataifa kuweka msimamo na kusaidia kukomesha biashara ya pembe za tembo na faru duniani. Kama hili litafanyika tembo na faru watakuwa salama.”

Ameongeza: “Wakati CITES ilipopiga marufuku biashara ya pembe za tembo mwaka 1989, hali hiyo ilisaidia kuongezeka kwa idadi ya tembo duniani. Naamini kuwa kama biashara hiyo itapigwa marufuku tena leo, matokeo yatakuwa yale yale. Maisha ya tembo na faru wengi yataokolewa na hatutakuwa na haja ya kuwa na wasiwasi.”

Rais pia ametoa mapendekezo mengine makuu manne kama njia ya kukabiliana na ujangili na biashara haramu ya pembe za ndovu ikiwa ni pamoja na ahadi kwamba Serikali itaendelea kuongeza nguvukazi ya maofisa na askari wanyamapori na kuhakikisha kuwa maofisa na askari hao wanapata mafunzo mwafaka ya kuifanya kazi hiyo.








All the contents on this site are copyrighted ©.