2014-02-14 08:34:24

Tafakari ya neno la Mungu, Jumapili ya VI ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa


Ninakuleteeni tena ujumbe wa Neno la Mungu katika Dominika ya VI ya kipindi cha mwaka A. Neno la Mungu latukumbusha kuwa Kristu Mwana wa Mungu hakuja kutangua Torati bali kuikamilisha. Kristo ni sheria mpya na hivi analeta ukamilifu wa sheria ya Mungu. Katika Somo la kwanza toka kitabu cha Yoshua bin Sira, Mungu anatangaza uhuru kamili kwa mwanadamu. RealAudioMP3

Anamtaka mwanadamu aamue mwenyewe kumchagua Mungu au kumchagua shetani! Anatumia alama za moto na maji, uzima au mauti akitaka mtu aone katika uhuru wake mwenyewe wajibu wa kuchagua jema au baya. Kwa hakika ni alama yakwamba mwanadamu alizaliwa akiwa huru na hivi matendo yote ya nje hayawi ya kutenda tu bali mwanadamu anawajibika kuchagua kwa kuwa anao uwezo huo. Kama anataka maisha ya kiroho basi atachagua amri za Mungu, kama anataka kifo cha kiroho basi atachagua rushwa na vionjo vya mwili!

Katika somo la II mtume Paulo anaendelea kuwasisitizia Wakorinto juu ya hekima ya Mungu yakuwa ni siri ambayo haikufunuliwa kwa watawala wa dunia bali ilifunuliwa kwa Mitume. Kwa kuthibitisha hilo anasema kama wangalipewa hekima hiyo wasingalimtundika msalabani Mwana wa Mungu. Ndiyo kusema hekima waliyonayo wakristu si hekima ya kawaida ya kidunia bali hekima ya kimungu. Ni hekima ambayo inakuja kwetu kwa njia ya mpango wa Mungu ulio wa milele. Siri ya hekima hii ni kwamba wanaijua wale waliokomaa katika imani na tumaini la kweli katika Kristo Yesu.

Katika somo la Injili , Mwinjili Matayo akinukuu maneno ya Bwana anasema sikuja kuondoa hata yodi moja wala nukta moja bali kuifanya sheria ya Mungu iweze kueleweka vizuri zaidi katikati ya watu. Nimekuja kuifanya sheria iwe kwa ajili ya watu wa Mungu yaani kuwajengea uhuru kamili.

Mpendwa msikilizaji, Bwana anao uwezo wa kutafsiri sheria katika mtazamo wa mapendo kwa watu. Ona jinsi anavyowapenda wanadamu na hata akathubutu hata kuivunja Sabato. Anachotafuta kwa uhakika ni kuipa sheria uwezo wa ndani unaozaa mapendo kwa mwanadamu. Sheria iliyokuwa kavu anaipa nyama na hivi inaweza kutafunwa kwa urahisi!

Anakazia pia maana na namna ya kutafsiri sheria, akitaka tusiishie katika kile kilichoandikwa katika mwonekano wa kawaida, mfano usiue, kwa namna ya kutambua kuua kama ile hali ya kuondoa maisha kimwili, bali tutazame ndani na kugundua kuwa hata wale walio na lugha chafu, hasira, chuki wanashiriki katika mauaji ya wenzao.

Anatoa mfano wa kunawa hata viwiko ulio utamaduni wa Wayahudi kabla ya kwenda Hekaluni kwa ajili ya kutolea sadaka, hili kwake halina maana kama mmoja haangalii moyo wake. Matendo haya ya kilitrujia hayatoshi kama hayaambatani na toba ya ndani na upatanisho na wenzetu. Bwana akisonga mbele na mafundisho yake anakazia amri ya ndoa yakwamba kadiri ya mpango wa Mungu ndoa haitenganishwi. Ndiyo kusema katika mantiki ya ndoa ya kudumu, yafaa kukazia maisha ya unyenyekevu ili kuweza kuhimili vitimbwi nyemelezi dhidi ya familia. Hii haina maana yakwamba wale walioanguka katika utengano wadharauliwe katika jumuiya bali waombewe daima kwa ajili ya mabadiliko yao ya ndani.

Mpendwa mwanatafakari, Bwana anazidi kufunua namna ambavyo mkristu anapaswa afanye anapojikuta mbele ya kutoa ahadi na kiapo. Anawaalika wakristu daima wawe ni watu wa kusema ukweli daima. Maneno yao yawe ya unyoofu, wasiishi undumilakuwili yaani katika mazingira fulani ndiyo na katika mazingira tofauti siyo kwa jambo lilelile. Hii ni sumu kwa familia na jumuiya kwa ujumla, ni sumu wa serkali na utawala wa nchi.

Basi mpendwa jaribu kufuata hatua kwa hatua mafundisho ya Bwana kwa ajili ya kukua kiroho katika tumaini la kweli litakalokupa uzima wa milele. Nikutakie furaha na matumaini katika kushika mausia ya Bwana ambayo ndiyo sasa dira kamilifu na itupayo uhuru kamili wa wana wa Mungu.
Tumsifu Yesu Kristo.
Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya, C.PP.S








All the contents on this site are copyrighted ©.