Maswali yaliyoulizwa na wanandoa watarajiwa kwa Papa Francisko
Katika Maadhimisho ya Siku ya Wapendao Duniani kwa Mwaka 2014, Baba Mtakatifu Francisko
amekutana na wanandoa watarajiwa 20, 000 kutoka katika nchi 28, waliokusanyika kwenye
Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ambao ulipambwa na kupambika
kwa sura za vijana wanaopendana, vijana ambao wanataka kufunga pingu za maisha, ili
kufurahia maisha hadi pale kifo kitakapowatenganisha.
Wanandoa wamemwambia
Baba Mtakatifu Francisko kuhusu: furaha ya maisha ya ndoa, wasi wasi na mashaka yaliyomo
mioyoni mwao. Uaminifu hadi kifo kitakapowatengenanisha ni kati ya changamoto kubwa
iliyoko mbele yao kutokana na ukweli kwamba, hata katika maisha ya ndoa na familia
bado kuna usaliti mkubwa ambao unapelekea ndoa nyingi kuvunjika au kukosa mwelekeo.
Vijana
wamemwambia Baba Mtakatifu kwamba, kati yao walikutana kwa mara ya kwanza wakati wa
Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani huko Madrid, Hispania, kila mtu akiwa amebeba
ndani mwa begi lake: sala, matumaini, udadisi na maswali yasiyokuwa na majibu. Walionana,
wakapendana na sasa wanataka kufunga ndoa Kanisani, ili kujenga familia ambayo kimsingi
ni Kanisa dogo la nyumbani. Vijana wanataka kusikia kutoka kwa Baba Mtakatifu: mtindo
wa maisha ya ndoa na familia ya Kikristo; tasaufi ya maisha ya ndoa katika ujumla
wake.
Wanandoa watarajiwa wamezungumzia kuhusu ushiriki wao mkamilifu katika
maisha na utume wa Kanisa mahalia. Baada ya kufahamiana, sasa wanasubiri kwa hamu
kubwa ile siku watakaposimama mbele ya Altare ili kufunga ndoa, kwa kuwa na kiasi
pasi na kutaka makuu; kwa kuonesha mshikamano wa upendo na maisha ya kujisadaka kwa
ajili ya wengine, kwa kutambua pia athari za myumbo wa uchumi kimataifa ambao umekuwa
ni kikwazo kikubwa kwa vijana wengi kufunga ndoa Kanisani. Ni vijana wenye matumaini
makubwa, lakini kuna wajanja wachache wanaotaka kuwapokonya matumaini yanayojikita
mioyoni mwao!